Michezo

Harambee Stars yarejea bila kocha, beki Mohamed aomba msamaha kusababisha bao

July 4th, 2019 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars imerejea nyumbani bila kocha Sebastien Migne mapema Alhamisi kutoka Misri baada ya kubanduliwa nje ya Kombe la Afrika (AFCON) kwenye mechi za makundi, huku beki Musa Mohamed akijitokeza kuomba mashabiki msamaha kwa kuchangia katika masikitiko hayo.

Kulingana na tovuti ya Goal, Migne aliamua kurejea nchini mwake Ufaransa kwa likizo ya juma moja kabla ya kujiunga na Stars ambayo italimana na Tanzania mnamo Julai 26 na Agosti 2 katika mechi za raundi ya kwanza za kufuzu kushiriki soka ya Afrika ya CHAN 2020.

“Migne ameamua kutembelea familia yake nchini Ufaransa kwa juma moja kabla arejee jijini Nairobi,” tovuti hiyo imenukuu afisa mmoja kutoka Shirikisho la Soka la Kenya (FKF), ambaye hakutaka kutajwa, akisema.

Naye beki wa klabu ya Nkana nchini Zambia, Musa Mohamed, ametaka Wakenya wamsamehe kwa masihara yaliyofanya Stars idhalilishwe 3-0 na Teranga Lions ya Senegal katika mechi yake ya mwisho ya Kundi C jijini Cairo hapo Julai 1.

“Makosa yalikuwa yangu. Sikumsoma vizuri Sadio Mane na akafikia mpira kabla mimi. Ningependa Wakenya wanisamehe. Ni hali ya mpira na hakuna kitu ningeweza kufanya baada ya kupoteza mpira. Natumai Wakenya watanisamehe. Naahidi kufanyia Kenya kazi nzuri nikipewa fursa tena,” alieleza tovuti hiyo baada ya timu hiyo kuwasili katika uwanja wa ndege wa Jomo Kenyatta saa tisa na nusu Alhamisi asubuhi.

Kenya ilishinda mechi moja nchini Misri baada ya kutoka chini mara mbili na kulima Tanzania 3-2 kupitia mabao mawili ya Michael Olunga na moja kutoka kwa Johana Omollo mnamo Juni 27.

Ilianza kampeni yake kwa kupoteza 2-0 dhidi ya Algeria.

Hii ilikuwa mara ya sita mfululizo Kenya haijapita mechi za makundi baada ya mwaka 1972, 1988, 1990, 1992 na 2004.