Michezo

Harambee Stars yarejea nchini baada ya matokeo ya kukera

March 29th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

HARAMBEE Stars imerejea nchini Alhamisi kutoka Morocco ambako ilisikitisha baada ya kumaliza mechi mbili za kirafiki bila ushindi dhidi ya limbukeni Jamhuri ya Afrika ya Kati (CAR) na Comoros.

Stars, ambayo inashikilia nafasi ya 105 duniani, ilikabwa 2-2 dhidi ya nambari 132 duniani Comoros hapo Machi 24 na kulemewa 3-2 dhidi ya nambari 121 duniani CAR mnamo Machi 27.

Matokeo haya yalishuhudia Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) likitangaza kumtimua kocha wa muda Stanley Okumbi pamoja na kocha msaidizi Frank Ouna na kocha wa makipa Hagai Azande.

Katika mechi ya kwanza dhidi ya Comoros, Kenya iliongoza 1-0 kupitia penalti ya kiungo wa Tottenham Hotspur Victor Wanyama baada ya kiungo Eric Johanna Omondi wa IF Brommapojkarna nchini Uswidi kuangushwa ndani ya kisanduku.

Wanavisiwa wa Comoros walisawazisha 1-1 kupitia Youssouf M’Changama dakika ya 20 kabla ya kuongoza 2-1 baada ya Djamel Bakar kuona lango dakika ya 73.

Mshambuliaji wa Buildcon nchini Zambia, Clifton Miheso alinasua Stars kutoka minyororo ya kupoteza mchuano huo aliposawazisha 2-2 zikisalia dakika sita kipenga cha mwisho kilie.

Katika mechi ya pili, ambayo Spurs ilikataa Wanyama achezeshwe, Foxi Kethevoam aliweka CAR bao 1-0 juu dakika ya 14. Omondi alisawazisha 1-1 baada ya kumegewa pasi murwa na mvamizi Michael Olunga (Girona, Uhispania).

Eudes Dagoulou alirejesha CAR mbele 2-1 dakika ya 63 kabla ya Hilaire Momi kuimarisha uongozi huo hadi 3-1 kupitia penalti.

Olunga alifungia Stars bao la pili dakika ya 87. Kenya ilimaliza mechi watu 10 uwanjani baada ya mzawa wa Uhispania, Mkenya Ismael Gonzalez kuonyeshwa kadi nyekundu.

Stars, ambayo inatarajiwa kupata mkufunzi wa kigeni kujaza nafasi ya Okumbi, ilitumia michuano hiyo kujiweka tayari kwa mechi ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika dhidi ya Ghana mwezi Septemba mwaka 2018. Kundi la Kenya pia liko na Sierra Leone na Ethiopia. Sierra Leone ilipepeta Kenya 2-1 katika mechi ya ufunguzi mwaka 2017.