Harambee Stars yarejea nyumbani na pointi moja kampeni ya kuingia Kombe la Dunia 2022

Harambee Stars yarejea nyumbani na pointi moja kampeni ya kuingia Kombe la Dunia 2022

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya Harambee Stars imerejea nyumbani Jumatatu baada ya kupiga sare ya 1-1 dhidi ya Amavubi Stars ya Rwanda kwenye mechi yake ya pili ya Kundi E ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 iliyosakatwa Septemba 5.

Vijana wa kocha Jacob “Ghost” Mulee walianza kampeni yao kwa kutoka 0-0 dhidi ya Uganda Cranes ugani Nyayo jijini Nairobi mnamo Septemba 2 kabla ya kuelekea Rwanda baadaye siku hiyo kwa mechi ya pili.

Mshambuliaji wa klabu ya Al Duhail, Michael Olunga, ambaye ni nahodha mpya wa Harambee Stars baada ya Victor Wanyama kustaafu kimyakimya, aliweka Kenya kifua mbele dakika ya 10 safu ya ulinzi ya Rwanda ilipozembea kuondosha hatari kufuatia kipa kutema mpira.

Hata hivyo, wenyeji Rwanda walitumia ikabu waliopata nje ya kisanduku pembeni kushoto kusawazisha 1-1 kupitia kwa Abdul Rwatubyaye dakika ya 21. Bao hilo lilitikisa Wakenya na hawakufaulu kuona lango tena.

Vijana wa Mulee walisababisha madhambi mengi, kunawa mpira mara kadhaa wakifanya mashambulizi na pia kukosa kuonana katika pasi zao nyingi.

Sasa, wanatupia jicho michuano miwili ijayo dhidi ya Mali itakayosakatwa kati ya Oktoba 6-9 ugenini na Oktoba 10-12 hapa jijini Nairobi. Ili kufufua matumaini yao ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya kufeli katika majaribio 13 mfululizo, vijana wa Mulee lazima wapige Mali.

Timu ya Mali imekaa juu ya jedwali kwa alama tatu. Mali walipata alama hizo kwa kunyuka Rwanda 1-0 mjini Agadir nchini Morocco mnamo Septemba 1.

Timu hiyo kwa jina la utani kama Eagles, itavaana na Uganda ugani St Mary’s Kitende hii leo Jumatatu katika mechi yao ya pili. Kenya ina alama mbili katika nafasi ya pili nao Uganda na Rwanda wamezoa alama moja kila mmoja.

Kuna makundi 10 ya timu nne nne katika raundi hii ya pili ya mashindano ya Bara Afrika ya kufuzu kushiriki Kombe la Dunia 2022 nchini Qatar. Washindi wataingia raundi ya tatu. Washindi wa mechi tano za muondoano za timu mbili mbili katika raundi ya tatu watajikatia tiketi ya kuwa Qatar.

You can share this post!

MBWEMBWE: Kiungo Di Maria ni mwenye guu la Almasi, ana...

Lori la polisi lagonga nyumba za mtaa wa mabanda