Michezo

Hargreaves asema ndoto ya Arsenal kumaliza Nne Bora haitatimia

April 3rd, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

KIUNGO wa zamani wa Manchester United Owen Hargreaves ameendeleza uchokozi wake dhidi ya Arsenal kwa kudai kwamba haiwezi kumaliza ndani ya mduara wa nne bora msimu wa 2018/19 wa Ligi Kuu ya Uingereza(EPL).

Kulingana na Hargreaves ambaye pia alisakatia Manchester City kabla ya kuangika daluga zake, fomu mbovu ya Arsenal katika mechi za ugenini ndiyo sababu kuu yao uwezekano wa kumaliza katika nafasi ya tatu au nne kuwa finyu.

Vijana wa kocha Unai Emery walipanda hadi nafasi ya tatu katika msimamo wa jedwali la Ligi Kuu(KPL) usiku wa Jumatatu Aprili1 kwa kurekodi ushindi wa kumi mfululizo wa mechi za nyumbani kwenye ligi ya EPL ugani Emirates. The Gunners walishinda mechi hiyo 2-0 dhidi ya Newcastle United huku Manchester United wakikaliishwa 2-1 na Wolves usiku wa Jumatano Aprili 2.

Hata hivyo, rekodi ya Arsenal katika mechi za ugenini imekuwa mbovu na hadi sasa wameshinda mechi tano tu kati ya 14 walizowajibikia ugenini msimu huu kwenye Ligi kuu.

“Nafikiri Man U na Tottenham Hot Spurs zitatinga nne bora huku Arsenal na Chelsea zikifungiwa nje kutokana na idadi ya mechi za ugenini watakazopambana nazo kabla msimu kufikia ukingoni,” akasema Hargreaves.

“Fomu ya Arsenal nyumbani ni nzuri sana ila wamekuwa wakiangukia pua katika mechi za ugenini. Spurs wamekuwa wakishinda mechi za ugenini na wana uwezo mkubwa wa kutwaa nafasi ya tatu ikilinganishwa na timu nyingine,” akaongeza.

Arsenal watapambana na Everton ugani Goodison Park Jumapili Aprili 7 kisha wavaane na Watford, Wolves, Leicester kabla ya kuwaandaa Burnley kwenye mechi ya mwisho ya msimu huu ugani Emirates.