Habari Mseto

Harmonize jikoni kuandaa kolabo ya kutisha akiwa na Nyanshinki

May 29th, 2018 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

MKALI wa nyimbo za Bongo, Harmonize anayetambulika kwa kupiga kolabo na wasanii, na kuibua vibao vinavyowavutia wapenzi wengi wa Bongo Afrika Mashariki, sasa anapanga kuangusha bonge la kolabo na msanii Mkenya hivi karibuni.

Kolabo zake akiwa na msanii wa humu nchini Willy Paul ‘Msafi’ na mwanabongo mwenzake Diamond Platnumz vimekuwa na wafuasi wake kwenye redio. mitandaoni na katika mfumo wa YouTube.

Akisema na redio moja ya mjini Mwanza, Tanzania msanii huyo amefunguka kuwa amekuwa akishauriana na msanii wa humu nchini mwenye sauti ya kuongoa, Nyashinki aliyerudi kwa ulingo wa usanii miaka michache iliyopita, na huenda hivi majuzi wakatoa kazi mpya itakayotetemesha anga za muziki Afrika Mashariki.

“Wajua kibao chenyewe hapa nikimuweka msanii fulani atafaa, kwa mfano,  juzi niliongea na Nyashinski tukapanga tufanye kolabo, akaniambia poa basi mwanangu angalia ngoma unitumie nirekodi, ’’ akasema Harmonize kwa lugha ya Kibongo.

Akijituma kwa kazi hiyo, sasa Harmonize anasaka wimbo utakaofaa kwa wawili hao kushirikiana huku akitaja kuwa kuna baadhi ya nyimbo ambazo hawezi kuzitumia kwa kuwa haziingiani na mbinu ya Nyanshinki ya usanii.

“Sasa nikawa najiuliza nimtumie wimbo gani, kila nikiangalia ‘store’ yangu naona daah, unajua kuna nyimbo nyingine unaona hapa hawezi kukaa kabisa yaani utakuwa unalazimisha. Ila bado nafikiria ni wimbo gani nikampa anaweza akafiti,’’ akaongeza.