Bambika

Harmonize sasa adai atakuwa daktari akistaafu muziki

Na WINNIE ONYANDO August 2nd, 2024 1 min read

STAA wa Bongo Flava, Rajab Kahali, almaarufu Harmonize, sasa anasema kuwa atasomea udaktari baada ya kustaafu kutoka kwa tasnia ya muziki.

Akizungumza kwenye mojawapo wa mahojiano, mwanamuziki huyo mashuhuri alisema kuwa anafahamu kwamba hatakuwa mwanamuziki milele na ndio maana ana nia ya kusomea udaktari.

“Nimekuwa nikifikiria kuhusu maisha yangu na ndio maana nataka kuwa daktari nikistaafu. Nitasomea kozi hiyo katika miaka yangu ya 45 au 50. Ningependa kutumia angalau mwaka mmoja kufanya kazi katika hospitali ili kusaidia watu,” Harmonize anasema.

Staa huyo alisherehekea miaka yake 30 ya kuishi duniani mwaka huu.

Tangu aanze kuimba, Harmonize amepata utajiri mkubwa kutokana na muziki wake na ana mpango wa kuendelea kuingiza mapato zaidi hadi umri wake wa kustaafu.

Msanii huyo alieleza kuwa licha ya kuacha shule akiwa Darasa la Saba kutokana na umaskini na kujishughulisha na muziki kama njia ya kuboresha maisha yake, kuwa daktari imekuwa ndoto.

Anaamini kuwa mabadiliko haya ya kazi yatamruhusu kusaidia jamii.

Hata hivyo, katika mojawapo wa mahojiano yake mwaka huu, mwanamuziki huyo alifichua kuwa tangu utotoni, ndoto yake haikuwa kuwa mwanamuziki bali kuwa mwanasoka mashuhuri.