Harrison Mwendwa katika rada kali ya AFC Leopards

Harrison Mwendwa katika rada kali ya AFC Leopards

Na CHRIS ADUNGO

AFC Leopards wamejitosa rasmi katika vita vya kuwania huduma za fowadi matata wa Kariobangi Sharks, Harrison Mwendwa, kadri wanavyolenga kukisuka upya kikosi chao kwa minajili ya kampeni za msimu mpya wa Ligi Kuu ya KPL.

Winga huyo wa zamani wa Mathare United, anahemewa pia na miamba wa soka ya Tanzania, Yanga SC ambao ambao pia wanafukuzia maarifa ya Sven Yidah wa Kariobangi Sharks na beki matata wa KCB na timu ya taifa ya Harambee Stars, Michael Kibwage.

Meneja wa timu ya Yanga, Dis Masten amekiri kuwa wanakaribia kutamatisha mchakato wa kusajili Yidah na Kibwage kabla ya kuwasilisha ombi rasmi la kumtwaa Mwendwa aliyewaridhisha sana wakati wa fainali za Super Cup zilizoandaliwa jijini Dar es Salaam mwanzoni mwa 2019.

Yanga almaarufu Jangwani Boys, tayari wanajivunia maarifa ya aliyekuwa kipa wa Bandari FC, Farouk Shikhalo.

Mbali na kuhusishwa pakubwa na Mwendwa, Leopards ambao ni mabingwa mara 13 KPL, wanawania pia maarifa ya nahodha wa zamani wa Gor Mahia, Harun Shakava, beki wa zamani wa Rayons Sports ya Burundi, Jules Ulimwengu na kiungo mzawa wa Uganda ambaye kwa sasa anavalia jezi za KCCA, Muzamiru Mutyaba.

Leopards wanapania pia kumrejesha kambini nahodha wao wa zamani Duncan Otieno anayeingia katika sajili rasmi ya Nkana FC nchini Zambia miaka miwili iliyopita.

You can share this post!

Kipande cha ardhi kilichokuwa kimenyakuliwa Thika...

COVID-19: Kenya yathibitisha vifo 12 idadi jumla ya...

adminleo