Harry Kane avunja rekodi ya Jimmy Greaves na kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Tottenham Hotspur kwa mabao 267

Harry Kane avunja rekodi ya Jimmy Greaves na kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Tottenham Hotspur kwa mabao 267

Na MASHIRIKA

FOWADI Harry Kane ametaka mashabiki kutarajia mabao mengi zaidi kutoka kwake baada ya kumpita nguli Jimmy Greaves na kuwa mfungaji bora wa muda wote kambini mwa Tottenham Hotspur.

Nahodha huyo wa timu ya taifa ya Uingereza alifunga bao lake la 267 akivalia jezi za Spurs mnamo Jumapili na kusaidia waajiri wake kukomoa Manchester City ambao ni mabingwa watetezi wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) 1-0.

Kane, 29, sasa analenga kuvunja rekodi ya kigogo Alan Shearer ambaye ni mfungaji bora wa muda wote katika EPL kwa mabao 260.

“Alan aliweka rekodi ambayo napania kuvunja. Najua Shearer atakuwa akinitazama katika kila mchuano ila sijui kama atafurahia mpango wangu huo. Ninachofahamu ni kwamba bado nina uwezo wa kufunga magoli mengi. Ninahisi vizuri sana,” akasema Kane ambaye sasa ana mabao 200 katika EPL.

“Washambuliaji katika mchezo wa soka wana tamaa. Hapana shaka kwamba Kane atataka mafanikio zaidi na kikubwa zaidi katika maazimio yake kwa sasa ni kufikia na kumpita Shearer,” akasema mvamizi wa zamani wa Crystal Palace, Bournemouth na Brighton, Glenn Murray, katika mahojiano yake na BBC.

Greaves, aliyeanza kusakata soka kambini mwa Chelsea, alipachika wavuni mabao 266 kutokana na mechi 379 akivalia jezi za Spurs kati ya 1961 na 1970.

Kwa upande wake, Kane alichezea Spurs kwa mara ya kwanza mnamo 2011 na amesakatia kikosi hicho jumla ya mechi 416 kufikia sasa. Bao lake dhidi ya Man-City mnamo Jumapili mbele ya mashabiki wa nyumbani ugani Tottenham Hotspur lilitokana na krosi safi aliyomegewa na Pierre-Emile Hojbjerg ndani ya kijisanduku.

Kane ndiye mchezaji wa tatu anayejivunia mabao mengi zaidi katika kipute cha EPL kilichoanzishwa mwaka wa 1992. Wanaomtangulia katika orodha hiyo ya wafungaji bora ni Shearer na Wayne Rooney ambaye alicheka na nyavu za wapinzani mara 208 akivalia jezi za Everton na Manchester United.

Kufikia sasa, Kane amefunga mabao 17 katika EPL na 19 katika mashindano yote ambayo amechezea Spurs. Hayo ni magoli 11 zaidi kuliko yanayojivuniwa na mfungaji nambari mbili kambini mwa Spurs, Son Heung-min.

Kane amesalia na bao moja pekee kuwa mfungaji bora wa muda wote katika timu ya taifa ya Uingereza. Kwa sasa anajivunia mabao 53 sawa na Rooney ambaye ni kocha wa DC United katika Major League Soccer (MLS) nchini Amerika.

Kane alizingirwa na kubebwa juu kwa juu na wachezaji wenzake baada ya mechi dhidi ya Man-City kabla ya kutoa hotuba fupi kwa mashabiki. Ujumbe wa pongezi kutoka kwa Danny ambaye ni mtoto wa marehemu Greaves pia ulionyeshwa kwenye viwambo ugani Tottenham Hotspur.

Baadaye katika chumba cha kubadilishia sare, Kane aliyekuwa bado ndani ya jezi yake, alipigiwa simu na kocha Antonio Conte aliyekosa mechi dhidi ya Man-City kutokana na upasuaji aliofanyiwa kwenye kibofu nyongo.

Licha ya mafanikio ya kufunga mabao mengi, Kane hajawahi kunyanyua taji lolote tangu aanze kuvalia jezi za Spurs utotoni. Aliwahi kuwaniwa pakubwa na Man-City mnamo 2021.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Kiangazi: Chemchemi za maji zakauka katika Kaunti ya...

Papa Francis akamilisha ziara yake Sudan Kusini

T L