Hasara, hofu ndovu wakivivamia vijiji

Hasara, hofu ndovu wakivivamia vijiji

Na MAUREEN ONGALA

WAKAZI wa Ganze na Magarini, Kaunti ya Kilifi wanaendelea kuishi kwa hofu baada ya ndovu kuvamia vijiji katika maeneo hayo.

Makundi ya ndovu kutoka mbuga ya wanyama ya Tsavo yametapakaa katika maeneo ya Kalongoni, Lwandani na Dingiria katika eneobunge la Ganze, na Shakahola, Degudegu na Kisiki eneobunge la Magarini.

Naibu chifu wa eneo la Chira, Bw Samwel Kitsao alisema ndovu hao ni wengi na imekuwa vigumu kwa wananchi kuwazuia.

“Ndovu wako kila mahali katika wadi ya Bamba. Kila mara habari za kuwa wanaonekana vijijini zinatufikia lakini imekuwa changamoto kwa wakazi kuwazuia kuvamia mashamba yao,” akasema.

Wanyama hao wameharibu mimea na pia kusababisha hofu ya kudhuru maisha ya wakazi.

Bw Dismus Ndoko kutoka kijiji cha Dingiria alisema kwamba ndovu hao pia hunywa na kuogea maji ya bwawa la pekee la Dingiria ambalo hutegemewa na wakazi wa lokesheni nne.

Sehemu nyingi za kutekea maji katika maeneo hayo zimekauka kutokana na ukame unaondelea kushuhudiwa katika kaunti hiyo.

Wakazi kutoka Jila, Mryachakwe, Mrima wa Ndege na Bungale hutegemea maji kutoka bwawa hilo.

Mara kwa mara, wakazi hulazimika kusubiri kwa umbali hadi ndovu hao watakapomaliza kunywa maji na kuoga kabla wao waende kuchota maji ya matumizi ya nyumbani.

Bw Ndoko asema wanafunzi kutoka shule za Bungale na Dingiria wameathiriwa baada ya kulazimika kutoenda shuleni mapema kwa kuhofia kuvamiwa.

Hali hii imewalazimu wazazi kusuburi hadi kupambazuke ndipo waandamane na watoto wao hadi karibu na shule ili kuhakikisha wako salama.

Bi Esther Kaliu, mfanyabiashara kutoka kijiji cha Bungale asema kuwa hulazimika kufungua duka lake lililoko katika soko la Dingiria kuchelewa kwani anaogopa kuvamiwa na ndovu anapotembea kutoka kwake kwani hupitia msituni.

Bw Emmanuel Baya, mwalimu wa shule ya msingi ya Kalongoni anasema baadhi ya wazazi wamewakataza watoto wao kuenda shuleni kwa kuogopa kuvamiwa.

Alieleza kuwa wakati mwingine wanaume hulazimika hupiga vibuyu vya maji na mabati ili kuwafukuza ndovu hao.

Bw Peterson Kazungu kutoka kijiji cha Bombi, Magarini alidai kuwa kuzungushwa kwa ua katika shamba kubwa la Galana–Kulalu ndicho chanzo kikuu cha ndovu hao kuvamia mashamba yao kutafuta chakula.

Shamba hilo la Galana–Kulalu lenye ekari milioni moja linatumiwa na serikali ya kitaifa kuendeleza mradi wa kupanda mahindi kwa njia ya unyinyizi maji.

“Ndovu walikuwa wanatoka katika mbuga ya Tsavo kula nyasi katika shamba hilo la Galana–Kulalu lakini kuzingirwa kwa shamba hilo kwa ua kumewafanya hawapati nyasi na maji na inawalazimu kuvamia mashamba yetu,” akasema.

You can share this post!

Helikopta iliyokuwa imembeba Raila yaanguka punde baada ya...

TAHARIRI: NHIF ifae maskini wanaougua corona