Habari Mseto

Hasara kwa wakulima mboga zao zikikosa soko

August 20th, 2020 1 min read

IRENE MUGO na FAUSTINE NGILA

Wakulima waliokuwa wakisambaza mboga shuleni wanakadiria hasara baada ya wanafunzi kubakia nyumbani kwa sababu ya mikakati iliyowekwa kudhibiti kusambaa kwa virusi vya corona.

Ni pigo kubwa kwa wakulima ambao kwa sasa wanauza kilo moja ya mboga kwa Sh3 kutoka Sh25 kabla ya corona.

Hasara zaidi ni kwamba mboga hizo zinalishwa mifugo kwa sababu ni rahisi kuharibika.

Shule zilifungwa Machi baada ya Kenya kuripoti kisa cha kwanza cha corona na sasa virusi hivyo vimeathiri watu zaidi ya 30,000.

“Nilifikiri shule zitafunguliwa baada ya muda mfupi lakini zimeendelea kufungwa huku matumaini yangu ya kupata faida yakiendelea kudidimia,” alisema Ben Nyaga, mkulima wa Mathira.

“Kupigwa marufuku kwa mikutano pia kumekuwa pigo kubwa kwangu. Tunauza kidogo kwa sababu zinaharibika haraka, zingine tunalisha ng’ombe na kugawia majirani,” alisema Bw Nyaga.