Hasara lori la unga wa Sh2.6 milioni likipata ajali karibu na hoteli ya Ole Sereni

Hasara lori la unga wa Sh2.6 milioni likipata ajali karibu na hoteli ya Ole Sereni

NA SAMMY KIMATU

BAADHI ya wakazi wa Nairobi leo Ijumaa wamechukua bure bila kulipia pakiti za unga wa ngano zilizoanguka na kutawanyika kote baada ya lori lililokuwa likiusafirisha unga huo kupata ajali.

Mkuu wa polisi eneo la Langata Bi Monicah Kimani amesema ajali hiyo ilitokea mwendo wa saa tano asubuhi.

Aidha Bi Kimani aliambia Taifa Leo kwamba lori hilo lilipoteza mwelekeo na kuanguka karibu na hoteli ya Ole Sereni mkabala wa barabara ya Southern Bypass.

Bi Kimani alitoa nambari za usajili wa lori husika kuwa ni KCN 027K.

Kando na hayo, alieleza kwamba dereva wa lori hilo alinusurika kifo kwa tundu la sindano lakini hakutoa maelezo zaidi.

Dereva alikuwa ametoka Mombasa kunakosagwa unga wa ngano aina ya Ajab na unga ulikuwa unapelekwa mjini Kisumu.

“Alikuwa ametoka Mombasa kunakosagwa unga huo na kampuni moja ili ausafirishe kuupeleka sokoni katika mji wa Kisumu wakati ajali ilitokea. Ajali ilitokea dereva alipotoka upande wa barabara kuu ya Mombasa Road kuingia Southern Bypass mwendo wa saa tano asubuhi karibu na hoteli ya kifahari ya Ole Sereni,” amesema kamanda Kimani.

Bi Kimani ameongeza kwamba unga huo ulikuwa umepakiwa robota 1,200 zenye thamani ya Sh2.6 milioni.

Hasara lori la unga wa Sh2.6 milioni likipata ajali karibu na Ole Sereni. PICHA | SAMMY KIMATU

Hata hivyo, amesema kabla ya maafisa wa polisi kuwasili katika eneo la tukio, hawakupata unga wowote ila kupata vumbi ya unga uliomwangika ukichanganyika na mchanga baada ya baadhi ya pakiti za unga kuraruka watu waking’ang’ania.

Lori lilikokotwa na kupelekwa katika kituo cha polisi cha Langata.

Kufuatia ajali hiyo, kulishuhudiwa msongamano mkubwa wa magari  baada ya wakazi wa Nairobi kufunga barabara ili wapore unga.

Baadhi ya wanaume wakibeba unga uliotawanyika baada ya lori kupata ajali karibu na hoteli ya Ole Sereni jijini Nairobi, Septemba 23, 2022. PICHA | JEFF ANGOTE

Katika kanda ya video iliyosambazwa mitandaoni, watu wanaonekana wakikimbia wakibeba unga kulingana na uwezo wa mtu binafsi.

Wengine walionekana wakiusafirisha unga waliopora kwa kutumia pikipiki.

Katika kanda hiyo pia, wanawake na watoto wanaonekana kukimbia kufika katika eneo la ajali angalau kuchukua pakiti moja ya bidhaa hiyo iliyo na bei ya juu madukani (zaidi ya Sh200 kwa pakiti moja).

Upande wa nyuma kwa umbali wa video, wanaume wasikika wakiongea wakikimbilia kuppora pakiti za unga.

Hali hiyo ilisababisha magari kwenda kwa mwendo wa kobe na kusababisha msongamano barabarani ya Mombasa .

Wakati huu bei ya pakiti moja ya unga inauzwa Sh200 baada ya serikali kusitisha bei ya awali ya Sh100 kwa kila pakiti ya unga wiki kadhaa zilizopita.

  • Tags

You can share this post!

Giroud akaribia rekodi ya mfungaji Thierry Henry nchini...

Bandari kuwakosa chipukizi wawili wenye majeraha mabaya

T L