Hasara upepo ukizidisha dhoruba Bahari Hindi

Hasara upepo ukizidisha dhoruba Bahari Hindi

NA KALUME KAZUNGU

WAVUVI katika maeneo ya Pwani wamepata hasara baada ya kushauriwa kutoenda baharini kwa sababu ya upepo mkali ukanda huo unaosababisha dhoruba katika Bahari Hindi.

Jumatatu, Idara ya Hali ya Hewa nchini ilitoa ilani kwa watumizi wa bahari katika Kaunti za Kwale, Mombasa, Kilifi na Lamu kusitisha shughuli zao kwa muda.

Uchunguzi uliofanywa na Taifa Leo katika Kaunti za Lamu, Kilifi, Kwale na Mombasa umebaini kuwa wavuvi wengi walikuwa hawajaenda kazini kwa siku tatu kufikia jana.

Wengi waliohojiwa walikiri kuteseka kwa njaa kutokana na ukosefu wa kazi baada ya kusitisha shughuli zao za uvuvi juma hili.

Mwenyekiti wa Muungano wa Vikundi vya Wavuvi (BMU), Kaunti ya Kilifi, Bw Charles Janji Nyale, alisema ingekuwa bora iwapo kuna njia za kuwasaidia wavuvi nyakati kama hizi.

“Tumeshuhudia wananchi wakifidiwa iwapo mimea yao katika maeneo ya nchi kavu imeharibiwa na wanyamapori. Kwa nini hawa wavuvi wetu hawafidiwi kila mara wanapopata hasara bahari ikichafuka? Kwa sasa hakuna kazi. Wavuvi wanahangaika na inasikitisha,” akasema Bw Nyale.

Kaunti ya Kilifi ina zaidi ya wavuvi 18,000.

Wavuvi

Katika Kaunti ya Lamu, karibu wavuvi wote 9,000 wanaopatikana eneo hilo wameathiriwa na dhoruba inayoendelea kushuhudiwa kwenye Bahari Hindi tangu wiki hii ilipoanza.

Mnamo Jumanne, mvuvi mmoja alifariki na wengine wawili wakaokolewa baada ya boti yao ya uvuvi kusombwa na mawimbi makali baharini na kuzama kwenye kisiwa cha Kiwayu, Kaunti ya Lamu.

Mwenyekiti wa BMU katika kaunti ya Lamu, Mohamed Somo alisema tayari kuna uhaba wa samaki kwenye mitaa ya Lamu.

Bei ya kilo moja ya samaki kwa sasa imepanda kwa kati ya Sh50 na Sh100, ambapo kilo moja inauzwa kwa kati ya Sh350 na Sh400 badala ya Sh300 bei ya kawaida.

“Wanunuzi ni wengi lakini wasambazaji hakuna. Isitoshe, familia nyingi zimebaki bila cha kufanya kwani tegemeo lao la kipekee ni uvuvi ambao hauwezi kutekelezwa kwa sasa,” akasema Bw Somo.

Katika Kaunti ya Kwale, hali ni ile ile ambapo wavuvi wamesalia nyumbani.

Naibu Katibu wa Muungano wa Wavuvi (BMU) eneo la Wasini, Bw Mohamed Kassim alisema mitaa mingi ya Kwale kwa sasa haina samaki kwani dhoruba kali inayoendelea baharini pia imefukuza hata samaki hao.

  • Tags

You can share this post!

Shahbal awapuuza wakosoaji

Vuguvugu kutoa mwaniaji ugavana

T L