Michezo

Hasenhuttl kusalia Southampton kwa miezi 4 zaidi

June 4th, 2020 1 min read

Na CHRIS ADUNGO

KOCHA Ralph Hasenhuttl ametia saini mkataba mpya wa miaka minne na Southampton katika makubaliano ambayo kwa sasa yatamsaza ugani St Mary’s hadi 2024.

Mkufunzi huyo mwenye umri wa miaka 52 na mzawa wa Austria alipokezwa mikoba ya Southampton mnamo Disemba 2018 wakati ambapo kikosi hicho kilikuwa kikining’inia padogo mkiani mwa jedwali na kuchungulia hatari ya kuteremshwa daraja. Katika msimu wake wa kwanza kambini mwa kikosi hicho, Hasenhuttl aliwasaidia Southampton kuponea chupuchupu.

Richard Kitzbichler ambaye ni msaidizi wa Hasenhuttl pia alirefusha muda wa kuhudumu kwake ugani St Mary’s kwa kipindi cha miaka minne.

“Maamuzi ya kurefusha muda wa kuhudumu kwangu kambini mwa Southampton yalikuwa rahisi kwa sababu nimejenga mahusiano bora na usimamizi wa klabu, wachezaji na mashabiki,” akatanguliza Hasenhuttl.

“Nilisema nilipowasili Southampton kwamba tulikuwa katika mwanzo wa safari ndefu. Tayari tumekuwa na matukio ambayo yametuhitaji kusherehekea pamoja, changamoto za kila sampuli na vitushi ambavyo vimeibua hisia mseto,” akaongeza.

Hadi kusitishwa kwa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), Hasenhuttl alikuwa ameongoza ufufuo wa kikosi chake na kuweka kando maruerue ya kichapo cha 9-0 walichopokezwa na Leicester uwanjani St Mary’s mnamo Oktoba.

Kichapo hicho kiliwasaza Southampton wakikodolea jicho hatari ya kushushwa ngazi. Kwa sasa, wanashikilia nafasi ya 14 jedwalini huku wakijivunia alama nne zaidi nje ya mduara hatari wa vikosi vitakavyoteremshwa daraja.

Kipute cha EPL kinatazamiwa kuanza upya mnamo Juni 17, 2020.