Habari

Hasira na majonzi dereva kuhepa baada ya kuua wanafunzi 10

August 6th, 2018 2 min read

Na WANDISHI WETU

HASIRA na majonzi zilitanda Jumapili kwenye kisa ambapo dereva wa trela alijaribu kutoroka baada ya kusababisha ajali iliyoua wanafunzi zaidi ya 10 katika Daraja la Kanginga, Mwingi, Kaunti ya Kitui.

Dereva huyo alikamatwa baadaye, akiwa zaidi ya kilomita 10 kutoka eneo la ajali ambapo wanafunzi hao wa Shule ya Msingi ya St Gabriel’s walikuwa wakitoka Mombasa kwa ziara ya kimasomo.

Ajali hiyo iliifanyika dakika chache kabla ya saa sita usiku, kilomita chache kutoka mahali ambapo wazazi walikuwa wakiwasubiri watoto wao.

Viongozi mbalimbali waliotuma risala za pole kwa familia, walisema vifo vya watoto hao havikustahili.

“Yasikitisha kwamba tulipoteza wanafunzi wachanga ambao bado hawakuwa wametimiza malengo yao maishani. Tunaomba wadau husika kuimarisha usalama wa wanafunzi ili kuepuka matukio kama hayo,” alisema Rais Uhuru Kenyatta kwenye ujumbe wake.

Kiongozi wa Wiper, Kalonzo Musyoka, aliwaomba wasimamizi wa shule mbalimbali nchini kutofanya safari za usiku.

“Matumaini ya watoto maishani hayakutimia. Wakati tunaomboleza mkasa huu, ninawaomba watumiaji wa barabara kuwa waangalifu zaidi,”alisema Bw Musyoka.

Gavana Charity Ngilu aliwaomba Wakenya kuziombea familia za walioathiriwa.

“Tuombe Mungu awalaze wanafunzi hao mahali pema peponi na kuzipa nguvu familia zilizoachwa,” akasema Bi Ngilu.

Mbali na viongozi, Wakenya kwenye mitandao ya Facebook na Twitter wakishinikiza waliohusika wachukuliwe hatua kali.

Kwenye mtandao wa Twitter, Mohamed Hersi alisema kiini kikubwa cha ajali huwa ni makosa ya kibinadamu.

“Lazima waliohusika wawajibike kwani, ni dhahiri huu ni ukosefu wa kuzingatia sheria za barabarani,” akasema.

Mukami wa Embu alieleza kufadhaishwa na ajali hiyo, akitaja kuwa “mkasa wa kitaifa.”

“Hii ni ajali mbaya sana. Waliokosa kuwajibika wakabiliwe kisheria,” akasema.

Kwenye Facebook, Margaret Wayua alisema si haki watoto kupoteza maisha yao. “Lazima sheria ifanye kazi,” akasema.

Jana, waziri wa Elimu Amina Mohamed aliwatembelea manusura katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta, Nairobi, alikosema kuwa wizara hiyo imewatuma maafisa wa elimu, ili kufuatilia hali za waathiriwa.

Kulingana na Bi Mohamed, kikosi hicho kitaongozwa na Mshirikishi wa Elimu wa eneo la Mashariki, ambapo kitashirikiana na idara zingine za seriiali.

“Kikosi kitahakikisha kuwa shughuli zote kuhusu ajali hiyo zimeendeshwa kwa njia ifaayo,” akasema.

Hata hivyo, alionya kwamba hatua kali zitachukuliwa wale watakaopatikana kukiuka kanuni zilizowekwa.

Mkuu wa Polisi wa Kitui ya Kati Muthuri Mwongera, ambaye aliongoza shughuli za uokoajii alisema wanafunzi wanane walifariki papo hapo baada ya kugongana ana kwa ana na trela lililokuwa likitoka upande wa pili.

Polisi walisema washamkamata dereva wa trela hilo, ambaye alijaribu kutoroka kuelekea Nairobi. Polisi walimkamata akiwa umbali wa kilomita 15 kutoka hapo.

Wanafunzi hao walikuwa miongoni mwa watu 50 waliokuwa wakisafiria basi hilo, ambapo walijumuisha walimu wao.

Kati ya waliojeruhiwa, wanafunzi 32 walilazwa katika Hospitali ya Mwingi Level Four, sita wakiwa katika hali mahututi, huku 26 wakiwa na majeraha madogo.

Wizara ilisema kuwa manusura walili wamelazwa katika Hospitali ya Kitaifa ya Kenyatta huku wengine wawili katika Nairobi Hospital.

Ilisema kuwa 23 miongoni mwao walitibiwa na kuruhusiwa kwenda nyumbani.

Ajali hiyo inatokea licha ya marufuku ya serikali dhidi ya safari za usiku za wanafunzi.

Marufuku hiyo ilitolewa na aliyekuwa Waziri wa Elimu Dkt Fred Matiang’i, kwa msingi wa kuhatarisha maisha ya wanafunzi. Marufuku hiyo pia ilichangiwa na ongezeko la ajali za barabarani kwa magari ya usafiri wa kawaida.

Boniface Mwaniki, Kitavi Mutua na Wanderi Kamau