Hasla bandia, Joshua feki 2022?

Hasla bandia, Joshua feki 2022?

MWANGI MUIRURI na BENSON MATHEKA

NAIBU Rais William Ruto amekashifiwa vikali kwa kutumia umaskini na matatizo yanayowakumba mamilioni ya Wakenya kwa maslahi yake ya kisiasa.

Wakosoaji wake wanahoji kauli yake ya ‘hasla’ kama iliyojaa unafiki kwani yeye sio wa tabaka hilo la maskini, mbali yeye ni bwanyenye.

Kwa Wakenya wa kawaida, ‘hasla’ ni mtu anayeng’ang’ana kutafuta mahitaji ya kimsingi kama vile chakula, mavazi na karo ya watoto.

Lakini Dkt Ruto anamiliki mali nyingi yakiwemo mashamba, majumba, biashara na mali nyingine ya thamani ya mamilioni, hivyo kuwa unafiki kwake kujiita ‘hasla’.

Mahasla wengi hawana ajira na wanafanya kazi za sulubu na hatari kama vile uchuuzi, matatu, kilimo katika vijishamba vidogo vidogo, vinyozi, saluni, jua kali miongoni mwa kazi zingine za mapato ya chini.

Tabaka hilo linajumuisha pia wakazi wa mitaa duni ya mabanda na mingine yenye misongamano, ambako huduma muhimu kama barabara na maji ni tatizo kupatikana.

Hii ni kinyume na Dkt Ruto ambaye anaishi mtaa wa kifahari wa Karen jijini Nairobi, huku washirika wake wa kisiasa ambao pia wanajiita ‘mahasla’ pia wakipatikana huko ama mitaa mingine ya hadhi kama Runda na Lavington.

Mahasla wengi hutembea kwenda kazini ama kutumia matatu, kinyume na naibu rais na washirika wake ambao husafiri kwa magari ya kifahari, baadhi ya thamani ya zaidi ya Sh20 milioni, na wanapoenda mbali hutumia helikopta.

RUTO ANAJALI ‘MAHASLA?

Lakini kunao wanaomtetea wakisema sio lazima kiongozi wa ‘mahasla’ awe yeye mwenyewe ni maskini kama wao

“Tunajua Ruto sio hasla, bali analenga kuwa kinara wa mahasla. Katika kufanya hivyo, wanaomwita mwizi na mfisadi wanafaa wamkamate na wamshtaki. Kauli nyingine yoyote ni kelele tupu ya kumpiga vita vya kisiasa,” asema mchanganuzi wa siasa, Prof Ngugi Njoroge.

Anaongeza kuwa ukipendwa kisiasa umependeka na hiyo ndiyo shida kuu iliyo na wapinzani wa Dkt Ruto kwa kuwa mbinu yake inawavutia ‘mahasla’.

Kulingana na Prof Ngugi, historia ya Dkt Ruto inaonyesha anawajali ‘mahasla’ kwani akiwa waziri ndiye alisukuma sera ya fatalaiza kwa bei nafuu, akathibiti bei ya ununuzi mahindi, akalainisha mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vikuu na pia akaondoa kozi zilizokuwa zikutumika kupuja wazazi pesa.

Lakini wengine wanatofautiana na kauli hiyo wanasema Dkt Ruto anapotosha mahasla.

“Dkt Ruto amejaribu sana kibinafsi kupanda hadhi kutoka umaskini hadi katika safu ya uongozi wa kitaifa. Lakini pale hasemi ukweli ni kudai kuwa mali hiyo ilitokana na uuzaji kuku na mayai.

“Tunapoambiwa kuwa aliuza kuku ndio akapata pesa za kujinunulia maekari ya mashamba na majumba ya kifahari katika kila pembe ya nchi tunafaa tujiulize ukweli wa madai hayo,” aliyekuwa mbunge wa Maragua, Bw Elias Mbau anasema.

Anaongeza: “Sio haki kuwapa vijana matumaini yasiyo na msingi kuwa unaweza ukauza kuku na mayai na uwe bilionea.”

Kauli hiyo inashikiliwa na Kinara wa Amani National Congress (ANC), Bw Musalia Mudavadi, ambaye amehoji iwapo kweli Dkt Ruto ni hasla na iwapo ushauri wake kwa vijana una msingi.

KUGAWA WAKENYA KITABAKA

Mchanganuzi wa siasa Prof Waswa Kisiangani kwa upande wake anakosoa ajenda ya kuwagawa Wakenya kwa misingi ya mapato au kikabila.

Anasema kuwa vuguvugu lolote linalodai kuwa na ajenda ya kuwasaidia wanyonge linafaa kueleza maono yake ya kuimarisha maisha ya Wakenya wote bila kujali kabila na tabaka.

Aliyekuwa mkuu wa mkoa, Joseph Kaguthi anashikilia kuwa kauli ya ‘hasla’ ni njama ya kisiasa ambayo inalenga kuwatumia wanyonge bila kutatua matatizo yao.

Bw Kaguthi anasema kauli hiyo inalenga zaidi watu wa jamii za GEMA katika Mlima Kenya na Rift Valley.

“Watu wengi wanaofanya kazi za pato la chini ni wa GEMA. Hivyo ukiwatafutia jina moja na uwaite ‘hasla’, utawaunganisha kwenye kapu moja na hivyo kuweza kuwatumia kufikia malengo yako ya kisiasa,” asema Bw Kaguthi.

Anahoji kuwa nembo ya Dkt Ruto ya wilbaro ni mbinu makusudi ya kulenga watu wa Mlima Kenya.

“Mbona nembo hiyo sio chombo cha kuvua samaki, kusafirisha mifugo au cha kuuzia ngano ama mahindi? Wilbaro ni chombo ambacho kinatumika katika kubeba vitu na wachuuzi ama mashambani, ambao wengi wanatoka Mlima Kenya,” asema.

Anasema hata kauli mbiu ya chama kipya cha United Democratic Alliance (UDA) kinachohusishwa na Dkt Ruto inatokana na usemi wa jamii ya Agikuyu “Wira ni Wira” (Kazi ni Kazi).

Kulingana na Bw Kaguthi vuguvugu la hasla limeundwa kwa nia pekee ya kumpa Dkt Ruto kura za Mlima Kenya kwenye uchaguzi wa 2022.

Nayo matukio na maamuzi ya kisiasa ya Kiongozi wa ODM Raila Odinga, yanaonyesha kuwa ahadi zake kwa Wakenya kwamba anajali maslahi yao huwa za uongo, wanahisi wataalamu.

Ingawa anaheshimiwa kwa kupigania demokrasia ya vyama vingi ikiwemo katiba mpya iliyopitishwa 2010, amekuwa akisaliti imani na matumaini ya wafuasi wake mara kwa mara licha yake kujiita ‘Joshua’ ama mkombozi wa wanyonge.

Wachanganuzi huru wa kisiasa wanasema ingawa Bw Odinga hajafaulu kuwa rais, maamuzi yake yanaonyesha hana tofauti na wanasiasa wengine nchini wanaotoa ahadi za uongo kuwasisimua wafuasi wao, na kisha kuwasahau wakipata mamlaka.

Wanasema lengo la Bw Odinga ni kujali maslahi yake binafsi, familia na washirika wake wa karibu.

“Matukio katika maisha ya kisiasa ya Bw Odinga yanadhihirisha hana tofauti na viongozi ambao amekuwa akikosoa akiwa katika upinzani. Japo wafuasi wake wanaamini kwamba akiwa rais anaweza kubadilisha uongozi nchini, hana tofauti na wengine. Nia yake huwa ni kuwatumia wafuasi wake kutimiza ajenda za kibinafsi,” asema David Wafula, wakili na mchanganuzi wa siasa.

Kwa kusukuma ajenda zake, Bw Odinga huchangia kugawanyika kwa Wakenya kwa misingi ya kikabila na kimaeneo, uovu ambao amekuwa akidai anapiga vita.

Bw Wafula anasema kabla ya siasa za vyama vingi kukubaliwa nchini, Bw Odinga alikuwa akilaumu na kukosoa vikali uongozi wa chama cha Kanu.

Lakini mnamo 2002 alivunja chama chake cha National Development Party (NDP), akaingia Kanu na kuteuliwa waziri katika serikali aliyokuwa akikosoa kwa ufisadi, utawala mbovu, ukiukaji wa haki za binadamu na ukabila.

“Kujiunga kwake na Kanu wakati huo kulimfungulia milango ya kuonja utamu wa kuwa serikalini japo wafuasi wake waliendelea kuteseka chini ya utawala wa Kanu,” asema Bw Wafula.

Kwa muda ambao alihudumu katika serikali ya Kanu akiwa waziri wa ujenzi, Bw Odinga hakukosoa sera zilizoporomosha uchumi kupitia ufisadi uliokithiri.

Baada ya Kanu kuondolewa mamlakani kwenye uchaguzi mkuu wa 2002 kupitia juhudi alizochangia pakubwa, Bw Odinga aliteuliwa waziri wa ujenzi na barabara hadi 2005 alipopinga kura ya maamuzi iliyonuiwa kubadilisha katiba.

Wachanganuzi wanasema aliyokuwa akipinga Bw Odinga mnamo 2005 ndiyo aliyounga mkono kwenye referenda ya 2010 akiwa waziri mkuu kwa sababu alidhani angeshinda urais Mzee Kibaki akiondoka mamlakani 2013.

“Alikuwa msitari wa mbele kupinga kura ya maamuzi ya 2005 akidai ilimpatia rais nguvu nyingi, lakini aliunga mkono ya 2010 iliyomwachia rais mamlaka hayo hayo kwa sababu alidhani ingemfaidi akishinda urais Mzee Kibaki akiondoka uongozini,” asema mdadisi wa siasa Joe Kanyi.

Bw Kanyi anasema kila wakati Bw Odinga akiingia serikalini huwa anasahau wafuasi wake na kuwakumbuka tu wakati wa kampeni anapowachangamsha na kuwasisimua kwa misemo ya kuvutia huku akijifanya mkombozi wao.

“Alipokuwa waziri mkuu, aliwasahau waliokufa na kufurushwa makwao kwenye ghasia za 2007, aliwateua watu wa karibu naye wakiwemo wa familia yake serikalini huku waliompigania wakiteseka. Hii inaonyesha kwamba ajenda yake kuu sio maslahi ya umma mbali ni yake binafsi,” asema Bw Kanyi.

Ingawa alikuwa akikosoa serikali ya Jubilee kwa ufisadi mkubwa, kupuuza utawala wa sheria na kulimbikiza madeni ya kigeni ambayo yamefanya maisha ya Wakenya kuwa magumu kupindukia, Bw Odinga alinyamaza alipoingia mwafaka na Rais Uhuru Kenyatta mnamo 2018, hatua iliyomfanya kusaliti mamilioni ya wafuasi wake ambao wakati wa kampeni za uchaguzi mkuu wa 2017 alikuwa amewaahidi kuwavukisha ‘Mto Jordan hadi Canaan’.

KUTULIZA BOLI

Mara baada ya kumezwa na Jubilee, Bw Odinga alituliza boli na kuanza kucheza ngoma ya Rais Kenyatta, mfano ikiwa ni hatua yake ya kuunga mkono ushuru wa VAT kwa petroli, akatetea maafisa wa serikali waliolaumiwa kwa wizi wa pesa za kukabili corona na kunyamaza polisi walipolaumiwa kwa kutumia nguvu kupita kiasi dhidi ya raia.

Wadadisi wanasema kuwa uchaguzi mkuu wa 2022 unapokaribia, Bw Odinga ameanza kutumia mbinu alizozoea za kujifanya mkombozi wa Wakenya kupitia mchakato wa BBI, ambao licha yake kudai unanuia kuunganisha Wakenya unatisha kugawanya nchi hata zaidi

Kulingana na Kasisi Mkuu Sammy Wainaina wa Kanisa la All Saints Cathedral, wanaosukuma BBI wanadanganya Wakenya kuwa itakuwa suluhisho kwa matatizo tele yanayowakumba wananchi.

“Sio ukweli kuwa BBI itatatua matatizo ya Wakenya. Huu ni mpango wa wanasiasa wachache kugawana madaraka. Mbona mwandanganya Wakenya? Iwapo mmeshindwa kupatia kaunti asilimia 15 ya bajeti, mtaweza vipi kuzipatia asilimia 35 mnazoahidi BBI ikipita?

“Mnaambiwa eti BBI ikipita viongozi wa kikabila watapata nafasi kuu za uongozi. Hata kama kinara wa kabila lako atakuwa pale juu, wewe mwananchi utaendelea kuwa maskini. Hata watu wa makabila ambayo yametoa marais wanaweza kukwambia ukweli kuwa hawajanufaika na hilo.

“Kile Wakenya wanataka ni ajira, afya bora, barabara, masoko ya kuuza mazao yao na usalama. Lazima tuzime ajenda ya wanasiasa ya kupora Kenya,” akasema Kasisi Wainaina.

You can share this post!

Manchester City waponda West Brom na kutua kileleni mwa...

LISHE: Ndizi na viazi