Habari

'Hasla' yatetemesha

October 9th, 2020 3 min read

Na WAANDISHI WETU

MBINU ya Naibu Rais William Ruto ya kujipigia debe miongoni mwa watu wa tabaka la chini imetia tumbojoto wapinzani wake na maafisa wa serikali, ambao sasa wameanza kumzima.

Hii ni baada ya Dkt Ruto kufanikiwa kupata umaarufu mashinani hasa miongoni mwa vijana na wanawake wasio na ajira, pamoja na wanaofanya kazi za malipo duni. Hii ni kupitia “ukarimu wake” kwao ambao umezaa vuguvugu la ‘Hasla’.

Kupitia mbinu hiyo, Dkt Ruto amekuwa akiwapa watu wachache vifaa vya kazi kama vile wilibaro, bodaboda, kufungulia baadhi biashara miongoni mwa hisani zingine.

Mnamo Jumatano, Mkuu wa Utumishi wa Umma Joseph Kinyua alimlaumu Naibu Rais akisema anatumia matatizo ya kiuchumi yaliyotokana na janga la corona kuwachochea vijana kwa itikadi kali. Hii ni licha ya kuwa kwa miaka mingi hata kabla ya corona, mamilioni ya vijana wamekuwa wakipitia magumu ya kimaisha kwa kukosa mbinu za kupata mapato ama kulipwa vibaya.

Kauli ya ‘Hasla’ imeibua dhana ya kuwepo kwa ushindani mkali kati ya maskini na matajiri, hali ambayo imezua wasiwasi wa kuchochea maasi ya kiraia ama Dkt Ruto kutumia wimbi hilo kushinda uchaguzi wa 2022.

Lakini Dkt Ruto amekosolewa vikali kwa kukosa kutumia madaraka yake kama Naibu Rais na nyadhifa zingine alizoshikilia awali kama vile waziri kuboresha maisha ya ‘mahasla’ ambao sasa anadai kuwatetea.

Wakosoaji wake wanasema kama angekuwa na nia njema kwa maskini, angepigania mifumo na miradi ya kuwainua kimaisha akiwa serikalini badala ya kuwapa wachache vifaa vya kazi huku mamilioni ya wengine wakiendelea kuteseka.

Lakini kutokana na matatizo mengi ya kiuchumi nchini na kupoteza matumaini maishani, vijana wasio na ajira wanamchukulia Dkt Ruto kama “mwokozi” wao, hatua ambayo haijawafurahisha wapinzani wake. Anaafikia haya kwa siasa zake za kujitambulisha kama ‘hasla’ ili kuvutia wengi wanaofurika kwenye mikutano yake kila pembe ya nchi.

Kwa kuhofia kampeni yake inaweza kuwachochea vijana kuzua maasi na pia kumjenga kisiasa, serikali sasa imeanza kutumia polisi na vyombo vingine vya usalama kuzima mikutano anayoandaa.

Hapo jana, polisi walisambaratisha ziara yake ambayo alikuwa amepangiwa kufanya katika eneo la Kebirigo, Kaunti ya Nyamira, ambapo alitarajiwa kuongoza hafla ya kuchangisha pesa kusaidia vyama kadhaa vya wahudumu wa bodaboda na makanisa.

Mamia ya polisi walifika katika uwanja wa Kebiringo na kuuzingira, huku wakiwaagiza wale wote ambao walikuwa wamefika kuondoka mara moja. Patashika kali ilizuka kati ya polisi na wakazi, polisi wakilazimika kutumia vitoa machozi kuwatawanya.

Kutokana na hali iliyotanda, Dkt Ruto alilazimika kufutilia mbali hafla hiyo hadi Alhamisi ijayo.

Kupitia ujumbe alioandika katika Twitter muda mfupi baada ya kizaazaa hicho, Dkt Ruto aliwalaumu polisi.

“Baada ya kufanya mashauriano na wabunge Vincent Kemosi (Mugirango Magharibi), Shadrack Mose (Kitutu Masaba) na Joash Nyamache (Mugirango Kaskazini), chama cha ushirika cha wanabodaboda na viongozi wa makanisa waliokuwa wametualika, tumeahirisha hafla mbili tulizopanga katika Kaunti ya Nyamira hadi Alhamisi wiki ijayo. Hatua ya polisi kuwaingilia Wakenya walioungana kuinuana kimapato ni ya kusikitisha,” akasema Dkt Ruto.

Hapo jana, makali ya serikali dhidi yake yaliendelea kudhihirika baada ya Baraza la Mawaziri kubuni kikosi maalum ambacho kitakuwa kikitekeleza kanuni za kiusalama zilizotolewa Jumatano na Baraza la Kitaifa la Ushauri kuhusu Usalama (NSAC).

Kwenye kikao na wanahabari mnamo Jumatano, Bw Kinyua alisema wanasiasa watalazimika kuwaarifu polisi kuhusu mkutano wowote wa kisiasa wanaolenga kufanya.

Kwa mujibu wa uamuzi wa Baraza la Mawaziri Alhamisi, kikosi hicho kitashirikisha Wizara ya Usalama wa Ndani, Afisi ya Mwanasheria Mkuu, Wizara ya Habari (ICT), Idara ya Ujasusi (NIS), Idara ya Polisi (ikiwa na wawakilishi kutoka Polisi wa Kawaida, Polisi wa Utawala na DCI), Tume ya Kitaifa ya Utangamano na Uwiano (NCIC) kati ya idara zingine.

“Lengo kuu la kikosi hicho litakuwa ni kufuatilia, kunakili na kutekeleza maagizo ya NSAC,” ikasema taarifa kutoka Ikulu.

Dkt Ruto na washirika wake wametaja mbinu hizo kama ishara ya kuonyesha wasiwasi miongoni mwa maafisa wakuu serikalini na washindani wake kisiasa.

Akihutubu kwenye makazi yake Jumatano, Dkt Ruto alitaja ghasia ambazo zilitokea katika Kaunti za Murang’a na Kisii kwenye ziara zake kama zilizopangwa.

Ripoti ya Benson Matheka, Wanderi Kamau na Ruth Mbula