Bambika

Hata kama mnaniita bikizee, mjue Guardian Angel ananipenda, asema Esther Musila

February 3rd, 2024 1 min read

NA FRIDAH OKACHI

MKE wa mwanamuziki wa nyimbo za injili Guardian Angel amewajibu wanaomkejeli kuwa atazeeka bila kujuta.

Wiki hii, wanamitandao wamekuwa wakichapisha picha ya familia yake na kuzua mjadala mtandaoni.

Picha hiyo inaonyesha Esther Ngenyi Musila, 53, akiwa amesimama mkono wa kushoto. Bintiye mwenye umri wa miaka 28 katikati na mwanamuziki Guardian, 32, akiwa amesimama upande wa kulia.

“Hapa kama watu wanadanganya yeye eti ‘love wins’ naona shida ya kiroho….Iko kitu kama mapenzi mahali?” aliuliza Gordon Opiyo.

Kwenye ukurasa wake wa Instagram, Bi Musila alitumia fursa hiyo kuonyesha dunia jinsi anasherehekea umri mkubwa akisema maisha ni baraka kutoka kwa Mungu. Pia alikashifu wale wanaokejeli wengine kuhusu umri wao akisema ataendelea kuzeeka bila kujuta.

“Watu wanapokutukana kwa sababu ya umri wako, huwa wanafikiri ni Mungu ndiye anayepeana uhai na si wao? Nitaendelea kuzeeka kwa uzuri na bila msamaha,” alisema Bi Musila.

Mama huyo wa watoto watatu pia, alifichua na kueleza jinsi alihudhuria mazishi ya marehemu aliaga wiki moja tu kabla ya siku yake ya kuzaliwa ya 50.

Alisimulia jinsi marehemu alitarajia sana kuhitimu umri wa miaka 50 lakini kwa bahati mbaya akaaga siku chache kabla ya kufika hapo.

“Leo asubuhi nilihudhuria ibada ya mazishi ya rafiki yangu. Leo ingekuwa siku yake ya kuzaliwa ya 50,” alisema kwa mafumbo.

Bi Musila alifunga pingu za maisha miaka miwili iliyopita na mwanamuziki Peter Omwaka almaarufu Guardian Angel. Ndoa ya wawili hawa imekuwa ikikosesha watu kadhaa amani na huwa mstari wa mbele kuwakosoa kutokana tofauti kubwa ya kiumri.