Makala

Hata mkiniita Zakayo, sijali chochote – Ruto

January 20th, 2024 1 min read

NA WANDERI KAMAU

RAIS William Ruto amesema kuwa yuko tayari kukosolewa kuhusu ushuru, badala ya kuruhusu Kenya kuzama kutokana na madeni.

Akihutubu Jumatano, alipokuwa akikagua Soko la Masinde Muliro mjini Kitale, Rais Ruto alisema kwamba atafanya kila awezalo kubuni ajira kwa vijana na Wakenya kwa jumla kupitia Mpango wa Ujenzi wa Nyumba za Bei Nafuu.

Akiwahutubia wakazi wa Kaunti ya Trans Nzoia, Rais Ruto alisema hajali kuitwa ‘Zakayo’, kwa hatua anazochukua kuzuia Kenya kuzama kwenye mzigo wa madeni inayodaiwa na mataifa ya nje na mashirika ya kifedha ya kimataifa.

“Nilisema tulipe Makato ya Nyumba, watu wakasema ninaleta mambo ya ‘Zakayo’. Heri mimi niwe ‘Zakayo’, lakini vijana wapate ajira. Heri niitwe ‘Zakayo’ na Kenya isiingie kwenye shimo la madeni,” akasema Rais Ruto.

Soma Utashuka tu, Raila amwambia Ruto kuhusu ushuru

Rais Ruto alipewa msimbo huo na Wakenya mnamo Mei mwaka uliopita, kutokana na sera zake kali za kuwatoza na kuwaongezea Wakenya ushuru.

Wakimpa jina hilo, watumiaji wa mitandao walimfananisha Rais na Zakayo kwenye Biblia, aliyepanda mti aina ya Mkuyu ili kumwona Yesu.

Kwenye Biblia, hasa Agano Jipya, Zakayo alikuwa mkusanya ushuru katika mji wa Yeriko.

Kulingana na simulizi za Biblia, Zakayo alichukiwa na Wayahudi kwa sababu walihisi alikuwa akijiwekea pesa alizokuwa akikusanya kama ushuru.

Hata hivyo, Rais Ruto amekuwa akionekana kutojali jina hilo, badala yake akisema “analikumbatia”.

Soma Mkopo mwingine: Wakenya kukamuliwa ushuru zaidi kulipa malimbikizi ya madeni

Pia Ruto: Sipunguzi ushuru ng’o!

Amekuwa akitetea sera za serkali yake kuhusu ushuru, akisema zina manufaa kwa nchi.

Alisema kuwa tatizo kuu linaloikabili Kenya si ushuru, bali madeni yake mengi.

Alisema madeni yameziletea baadhi ya nchi barani Afrika matatizo ya kiuchumi.

“Hakuna taifa lolote lililoharibiwa na ushuru. Badala yake, ninajua nchi nyingi zilizojengwa kwa ushuru,” akasema Rais Ruto.