Habari Mseto

Hatari ya kujianika mitandaoni msimu huu wa Krismasi

December 22nd, 2019 1 min read

Na MWANDISHI WETU

WAKATI wa msimu wa Krismasi, watu wengi huzama kwenye sherehe na kusahau usalama wao na mali yao.

Hata hivyo, mtaalamu wa masuala ya usalama, Tony Sahni, ambaye ni mkurugenzi wa kampuni ya usalama ya Securex anatoa mwongozo ambao watu wanapaswa kutumia kuhakikisha usalama wao, watoto na mali yao.

Bw Sahni anatahadharisha watu dhidi ya kutangaza mahali walipo msimu huu katika mitandao ya kijamii akisema, habari hizo zinaweza kutumiwa na wahalifu kuwalenga: “Kuwa mwangalifu kuhusiana na jumbe unazoweka katika mitandao ya kijamii.

Kwa mfano, ukisema uko mahali ambapo ni mbali na nyumba yako, wakora wanaweza kuvamia nyumba na kupora mali,” asema Bw Sahni.

Wakati huu wa Krismasi ni muhimu kuhakikisha nyumba yako na vitu vilivyomo ni salama. Hakikisha milango na madirisha ya nyumba yamefungwa nyakati zote ili wezi wasiingie. na kuiba.

Ikiwezekana, weka ving’ora, kamera za usalama (CCTV) na taa za usalama. Vile vile, uwe mwangalifu kuhusiana na jumbe unazoweka katika mitandao ya kijamii.