HabariSiasa

Hatari zawakodolea raia macho kutoka pande zote

November 12th, 2019 2 min read

Na VALENTINE OBARA

MBALI na kukabiliwa na hatari ya magonjwa yanayosababishwa na kula vyakula vyenye sumu, Wakenya pia wanakumbwa na matatizo mengine kutokana na ufisadi na maafisa wa serikali kuzembea katika kazi yao.

Changamoto hizi ni pamoja na usalama kutoka vijijini hadi mijini, magenge ya wahalifu yanaendelea kuzua wasiwasi kwa wananchi.

Mkenya hana amani anapotembea njiani, akijiburudisha katika mikahawa, akiwa kazini au hata akipumzika nyumbani na familia yake kwani anatambua kuna uwezekano mkubwa kushambuliwa wakati wowote na majambazi wenye silaha.

Cha kutia hofu zaidi ni kwamba, kumeibuka mtindo ambapo maafisa wa polisi ni washirika katika magenge hatari ya uhalifu hivyo kufanya raia kukosa pa kukimbilia.

ElimuWakati mzazi anapompeleka mtoto wake shuleni, matumaini yake huwa ni kwamba atakamilisha masomo katika mazingara salama ili kupata maisha bora miaka ya usoni.

Lakini hali sivyo kwani wazazi wengi huwa na wasiwasi muda wote ambapo mtoto yuko shuleni, iwe ni shule ya kutwa au ya mabweni kuanzia chekechea hadi vyuo vikuu.

Ripoti za walimu wanaoshambulia watoto, kuwabaka na kuwalawiti hujaa katika vyombo vya habari kila kukicha.

Kando na haya, kuna ripoti za walimu ambao husababishia watoto majeraha ya kudumu kwa kuwaadhibu kwa njia za kikatili.Kumekuwepo visa vya mabweni ya wasichana kushambuliwa na wahuni.

Wanafunzi wasio na nidhamu nao huhatarisha maisha ya wenzao wanapowasha moto kwa mabweni au kushambulia wenzao na kuwajeruhi.

Jana, kuliibuka kisa ambapo watahiniwa kadhaa wa Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE) walisemekana kuugua baada ya kutumia kemikali yenye sumu katika mtihani wao wa Kemia mnamo Ijumaa iliyopita.

Ghasia za kisiasaUchochezi wa kisiasa hufanya wananchi kukosa amani katika maeneo wanakoishi pembe tofauti za nchi.

Ghasia za baada ya Uchaguzi Mkuu wa 2007 zilitajwa kuwa mbaya zaidi za kisiasa kuwahi kushuhudiwa tangu Kenya ilipopata uhuru.Matarajio yalikuwa kwamba baada ya kupitisha katiba 2010, hali ya kisiasa ingebadilika.

Lakini maafa ya kisiasa yasiyonusuru hata watoto wachanga yakashuhudiwa tena katika uchaguzi uliopita mwaka wa 2017.

Ijapokuwa matumaini yalifufuliwa kwamba mwafaka wa Rais Uhuru Kenyatta na Kiongozi wa ODM Raila Odinga ungebadili mbinu za kisiasa nchini, uchaguzi wa wiki jana Kibra na ule wa wadi ya Ganda katika Kaunti ya Kilifi zilionyesha kuwa mambo bado ni kama zamani.

UmaskiniGharama ya juu ya maisha, madeni yanayokumba taifa, ufisadi na ukosefu wa ajira ni miongoni mwa masuala yanayokosesha wananchi usingizi.

Bei ya bidhaa muhimu imekuwa ikipanda na kufikia sasa, unga wa mahindi wa kilo mbili imefika zaidi ya Sh130.

Makampuni mengi yamefungwa wamiliki wakilalamikia hali ngumu ya kufanya biashara Kenya. Hii imefanya maelfu ya raia kufutwa kazi.

Wakenya wangali na wasiwasi kuhusu deni la taifa ambalo limefika Sh6 trilioni, huku bunge likiruhusu serikali kuendelea kukopesha hadi Sh9 trilioni.

UchukuziMaelfu ya wananchi hupoteza maisha yao ajalini kila mwaka, huku baadhi ya wanaonusurika wakiachwa na majeraha ya kudumu.

Hali hii imefanya raia asiwe na uhakika kuhusu maisha yake kila anapotembea, akiabiri gari la kibinafsi, la uchukuzi wa umma, bodaboda, feri au hata ndege.

Takwimu za Mamlaka ya Kitaifa ya Usalama na Uchukuzi (NTSA) zinaonyesha watu 2,326 walifariki kwenye ajali za barabarani mwaka huu kufikia Septemba.

Mojawapo ya chanzo huwa ni uendeshaji magari mabovu ambayo huruhusiwa barabarani na polisi au maafisa husika wa uchukuzi walio fisadi.

Kwa uchukuzi wa feri, kisa cha gari kuzama katika kivukio cha Likoni, Kaunti ya Mombasa mnamo Oktoba kilifichua hatari ambayo wasafiri wanaotegemea kivukio hicho hupitia kila siku.

Hali si tofauti katika anga za Kenya, kwani katika siku za hivi majuzi, kumekuwa na visa kadhaa vya ndege kuanguka au kupata hitilafu zikiwa angani.