Siasa

Hatima ya Jumwa, Wamalwa yaamuliwa

May 28th, 2020 2 min read

Na WAANDISHI WETU

MRENGO wa upinzani Nasa umeidhinisha kutimuliwa kwa wabunge wake waasi kutoka nyadhifa za uongozi katika bunge la kitaifa na uanachama wa kamati mbalimbali.

Na kiongozi wa ANC Musalia Mudavadi na mwenzake wa Ford Kenya Moses Wetang’ula wamekosoa hatua hiyo wakidai ilitekezwa na chama cha ODM bila vyama vyao kushauriwa.

Mkutano wa kundi la wabunge wa vyama tanzu vya muungano huo (PG) ulioongozwa na kiongozi wa wachache John Mbadi ulifikia kwa kauli moja hatua ya kumvua Mbunge wa Kiminini Chris Wamalwa (Ford Kenya) wadhifa wa naibu kiranja wa wachache. Nafasi hiyo imejazwa na mwenzake wa Tongaren Dkt Eseli Simiyu.

Naye Mbunge wa Likoni Mishi Mboko (ODM) ndiye mwakilishi mpya wa ODM katika Tume ya Huduma za Bunge (PSC) baada ya mwenzake wa Malindi Aisha Jumwa kupokonywa nafasi hiyo yenye hadhi kuu.

Na jumla ya wabunge wengine wanane wa vyama tanzu vya muungano huo waliondolewa kutoka nafasi wanazoshilikia kama wanachama katika kamati mbalimbali za bunge kwa madai kuwa “wamekuwa washirika wa vuguvugu la Tangatanga.”

“Wabunge hawa wamesimamishwa kama wanachama wa kamati zao kwa kipindi cha miezi sita ili tuone ikiwa watajirekebisha na kurejea katika mkondo unaotakiwa. Wale ambao wataendelea kuwa waasi watafungiwa nje kabisa,” kiranja wa wachache Junet Mohamed amewaambia wanahabari katika majengo ya bunge Alhamisi baada na mkutano huo.

Mbunge wa Butere Tindi Mwale (ANC) ameondolewa kutoka kamati ya bunge kuhusu Kawi, Sheria Mbadala na Kamati ya Uteuzi huku Silvanus Osoro (Mugirango Kusini, KNC) akipoteza nafasi yake katika kamati za Kilimo na Utekelezaji Maamuzi ya Bunge.

“Wabunge hawa tuliowaondoa wamedhihirisha kwamba sio waaminifu kwa sera na maongozi ya muungano wa Nasa. Baadhi yao wamekuwa wakikwepa kuhudhuria vikao vya kamati wakitumia muda wao mwingi kuzunguka mijini bila sababu maalum,” akaeleza Bw Mohamed ambaye pia ni mbunge wa Suna Mashariki.

Sasa, Bw Mudavadi amesema mabadiliko hayo yalifaa kuidhinishwa katika Kamati ya Vinara Wakuu wa Muungano wa Nasa (Summit).

“ODM haikufaa kutekeleza mabadiliko kama haya kwa njia ya kidikteta jinsi hii. Maamuzi kama haya yanafaa kufanywa na sisi kama vinara wenza katika muungano huu,” amesema.

Akaongeza: “Mabadiliko katika uongozi na uanachama wa kamati za bunge hayana budi kufanya kulingana na sheria za bunge pamoja na makubaliano ya wanachama wa vyama husika. ODM ina haki ya kufanya mabadiliko kuhusu wabunge wao lakini sio kuwaadhibu wabunge wa ANC.”

Naye Bw Wetang’ula ambaye alipokonywa wadhifa wa kiongozi wa wachache katika Seneti na ODM mwaka 2019 amesema hatua hiyo inaonyesha kuwa ODM haiheshimu vyama tanzu katika Nasa.

“ODM imekatalia fedha za kutoka hazina ya vyama vya kisiasa na sasa inaendelea kuadhibu wabunge wetu bila sababu. Hii sio haki,” amesema.

Na akijitetea Dkt Wamalwa amesema kuwa amekuwa akishirikiana na Naibu Rais Dkt  William Ruto katika masuala ya ujenzi wa Kanisa pekee katika eneobunge lake wala sio masuala mengine ya kisiasa.

Ripoti ya CHARLES WASONGA, DERICK LUVEGA na BENSON AMADALA