Habari Mseto

Hatima ya kesi inayohusu Matiang'i ni Ijumaa

November 25th, 2020 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA itaamua hapo Ijumaa iwapo itamruhusu mkurugenzi wa zamani wa mawasiliano ya dijitali ikuluni, Bw Dennis Itumbi, kumshtaki Waziri wa Usalama, Dkt Fred Matiang’i.

Bw Itumbi anataka kumshtaki waziri huyo kwa madai ya ufisadi kuhusu kashfa ya ununuzi wa shamba lenye thamani ya Sh1.5 bilioni katika eneo la Ruaraka, Kaunti ya Nairobi.

Hakimu Mkuu wa mahakama ya kesi za ufisadi, Bw Douglas Ogoti alisema atasoma ombi la Bw Itumbi kisha abaini ikiwa limetimiza vipengee vya sheria kuhusu kesi zinazowasilishwa kortini na watu binafsi kabla ya kutoa mwelekeo.

Katika ombi lake, Bw Itumbi anaomba mahakama imruhusu kumshtaki Dkt Matiang’i kwa madai ya kushiriki katika ufisadi wakati wa ununuzi wa shamba kutoka kwa Bw Francis Mburu.

Bw Itumbi hajawasilisha ushahidi wowote mbele ya mahakama kuhusu madai yake dhidi ya Dkt Matiang’i, akisema anasubiri mwelekeo wa mahakama kabla ya kufanya hivyo.