Habari Mseto

Hatima ya Obado, Oyamo, Obiero, Jacque na Jowie

October 23rd, 2018 1 min read

Na RICHARD MUNGUTI

GAVANA wa Migori Okoth Obado na washukiwa wengine wawili watajua hatima yao ya dhamana Jumatano huku mtangazaji Jacque Maribe na mchumbawe Jowie wakitazamiwa kuwasilisha ombi lao la kuachiliwa kwa bondi.

Jaji Jessie Lesiit atatoa uamuzi ikiwa Bw Obado, aliyekuwa msaidizi wake Bw Michael Oyamo na katibu wa kaunti Bw Caspal Obiero wataachiliwa huru kwa dhamana au wataendelea kukaa ndani hadi kesi dhidi yao ya mauaji isikizwe na kuamuliwa.

Watatu hao walikana kumuua mwanafunzi wa chuo kikuu cha Rongo Bi Sharon Beylne Otieno  na mtoto wake mnamo Septemba 3 2018 katika eneo la Owade, kaunti ndogo la Rachuonyo kaunti ya Homabay.

Upande wa mashtaka ulipinga Mabw Obado, Oyamo na Obiero wakiachiliwa kwa dhamana kwa madai watavuruga mashahidi kwa vile wanajua adhabu ya kosa wanayoshtakiwa ni kifo.

“Bw Obado yuko na ushawishi mkubwa na inahofiwa atawavuruga mashahidi wasifike kortini kutoa ushahidi kwa vile anajua adhabu ya mashtaka yanayomkabili ni kali,” alisema kiongozi wa mashtaka Bw Jacob Ondari.

Mawakili  Jaji (mstaafu) Nicholas Ombija , mawakili  Cliff Ombeta , Roger Sagana na Collins Ario waliomba mahakama imwachilie kwa dhamana wakisema ni haki ya kila mshukiwa kuachiliwa kwa dhamana hata ikiwa anakabiliwa na kesi ya aina gani.

Jaji Ombija na Bw Ombeta walisema upande wa mashtaka haujawasilisha sababu za kutosha kuwezesha mahakama kuwaachilie kwa dhamana washtakiwa.

Bi Maribe anayeshtakiwa pomoja na Bw Joseph Kuria Irungu almaarufu Jowie wanaoshtakiwa kwa mauaji ya Monica Nyawira Kimani wamewasilisha maombi waachiliwe kwa dhamana wakisema “hawatawavuruga mashahidi.”

Jaji James Wakiaga atasikiza ombi lao Jumatano. Kufikia sasa, wamekanusha shtaka dhidi yao.