Hatima ya Waiguru kujulikana Juni 26

Hatima ya Waiguru kujulikana Juni 26

Na CHARLES WASONGA

HATIMA ya Gavana wa Kirinyaga Anne Mumbi Waiguru sasa itajulikana Ijumaa wiki ijayo Juni 26 kamati maalum iliyoteuliwa kuchunguza tuhuma dhidi yake itakapowasilisha ripoti yake kwa Seneti.

Akiongea na wanahabari Jumatano baada ya kuchaguliwa kuwa mwenyekiti wa kamati hiyo, Seneta wa Kakamega Cleophas Malala alisema wawakilishi wa bunge la kaunti ya Kirinyaga watawasilisha ushahidi wao mbele ya kama hiyo Jumanne.

Kisha Jumatano Gavana Waiguru atafiki mbele ya kamati hiyo ya wanachama 11 kujitetea kabla ya kamati hiyo kufanya kikao cha faragha kuandaa ripoti yake ya mwisho.

Bw Malala alihakikishia umma na pande zote husika katika suala hilo kwamba kamati yake itahakikisha kuwa kamati hiyo itaendeshwa majukumu yake kwa haki, uwazi na kwa kuzingatia sheria.

“Tunafahamu fika kwamba suala hili limefuatiliwa kwa makini na Wakenya wote; kando na watu wa Kirinyaga. Kwa hivyo, tunawahakikishia kuwa tutaendesha kazi hii kwa haki na uwazi. Pande zote husika zitapewa muda tosha wa kutetemea misimamo yao mbele yetu,” akasema Seneta huyo wa ODM ambaye ni naibu kiongozi wa wachache katika Seneti.

Seneta Maalum Abshiro Halake (Kanu) alichaguliwa kuwa naibu mwenyekiti baada ya kumbwaga Seneta wa Nyandarua Mwangi Githiomi.

Mnamo Jumanne, juhudi za baadhi ya maseneta kutaka mashtaka dhidi ya Gavana Waiguru yashughulikiwe katika kikao kizima cha seneti bali sio katika kamati maalum, zilifeli baada ya wenzao wanaunga mkono handisheki kuwapiga kura ya kupinga wazo hilo.

Hiyo ilionekana kama ushindi wa kwanza dhidi ya mahasimu wa Bi Waiguru, na viongozi wa Kirinyaga, wanaohisi kuwa kuna uwezekano wa kuingiliwa watu fulani wanaotaka gavana huyo anusurike.

Maseneta hao wakiongozwa na Kipchumba Murkomen (Elgeyo Marakwet) na Charles Kibiru (Kirinyaga) walioelezea hofu kwamba wakereketwa wa handisheki na BBI “watatumia kamati hiyo kumtaka Gavana Waiguru na hivyo kuwanyima wakazi wa Kirinyaga haki.”

Tayari chama cha ODM kimemtetea gavana huyo sawa na Waziri wa Utumishi wa Umma Profesa Margaret Kobia, Katibu Mkuu wa COTU Francis Atwoli miongoni mwa wengine

Bunge la Kaunti ya Kirinyaga lilipitisha hoja ya kung’oa mamlakani Gavana Waiguru kwa tuhuma za kutumia vibaya mamlaka ya afisi yake na ukiukaji wa sheria za ununuzi kwa kutoa zabuni kinyume cha sheria. Pia madiwani hao walidai gavana huyo alitumia Sh10 milioni akidai ni marupurupu ya usafiri ilhali hakuenda popote.

You can share this post!

Kazi ya uchifu yaepukwa Lamu kutokana na mauaji

Echesa asirudishiwe silaha wala gari – DPP

adminleo