Siasa

Hatima ya Waiguru ni seneti lakini yeye afika mahakamani kupinga kuondolewa kwake

June 10th, 2020 1 min read

SAMMY WAWERU na MAUREEN KAKAH

SPIKA wa bunge la seneti Ken Lusaka amethibitisha Jumatano kwamba amepokea barua ikielezea hoja ya kumtimua Gavana wa Kirinyaga Anne Waiguru ambayo ilipata uungwaji mkono unaotosha.

Waiguru analaumiwa kwamba ana mienendo mibaya na anatumia afisi vibaya.

Jumanne, madiwani 23 kati ya 33 walipitisha hoja ya kumng’oa gavana Waiguru licha ya kuwepo kwa amri ya mahakama iliyozuia kujadiliwa kwake.

Akithibitisha kupokea hoja hiyo iliyowasilishwa kwake na spika wa bunge la Kirinyaga Antony Gathumbi, Bw Lusaka Jumatano katika kikao na wanahabari katika afisi yake Nairobi, aliwaambia kuwa tayari imepokezwa timu ya wanasheria.

“Tumeipokea na kuikabidhi kikosi cha wanasheria baada ya kuikagua Kwa sasa wanapaswa kuanza kuishughulikia,” Spika Lusaka akasema.

Gavana huyo wa zamani Bungoma, alisema amethibitisha nakala ya hoja hiyo, pamoja na sahihi za madiwani walioipitisha.

Ikizingatiwa kuwa seneti inajukumika kufuatilia utendakazi wa serikali za ugatuzi, alihakikisha kuwa bunge hilo litasikiliza pande zote mbili na uamuzi wa haki na uwazi kutolewa.

“Seneti ni bunge adilifu; Ni kama korti. Tutasikiliza pande zote mbili, pia tutampa gavana nafasi ya kujieleza na kujitetea. Madiwani wamefanya jukumu lao kama walinzi wa serikali ya kaunti,” Bw Lusaka amesema.

Hoja yenyewe inajiri wakati ambapo taifa linapambana na janga la Covid-19, na baadhi ya viongozi wanawake nchini wamejitokeza kukashifu hoja hiyo, wakidai inalenga kuduwaza uongozi wa wanawake nchini.

Spika Lusaka anatarajiwa kuteua kamati ya muda ya maseneta watakaojadili hoja hiyo.

Wakati huo huo, Waiguru amefika mahakamani kupinga kuondolewa kwake na bunge la Kaunti ya Kirinyaga.

Anasema ni hatua inayokiuka sheria kwa sababu mahakama kuu ilikuwa imesitisha japo kwa muda mchakato wa kumuondoa mamlakani kwa sababu ya changamoto za janga la Covid-19.

Endapo kamati hiyo itaridhishwa na uamuzi wa bunge la Kirinyaga, Waiguru atatemwa kama gavana, sawa na ilivyoshuhudiwa kwa aliyekuwa gavana wa Kiambu Ferdinand Waititu.

Waiguru hata hivyo, anaweza kuelekea mahakamani kukata rufaa.