Hatimaye Bomet yauza majanichai Iran

Hatimaye Bomet yauza majanichai Iran

Na VITALIS KIMUTAI

GAVANA wa Bomet Hillary Barchok hatimaye jana aliongoza maafisa wa Kaunti hiyo kuuza tani 84 za majanichai moja kwa moja kwa serikali ya Iran.

Hii ni baada ya majaribio ya kuuza majanichai hayo kutibuka mara tatu tangu Januari 25 mwaka huu. Mauzo hayo yamefanyika baada ya mahakama juzi kutoa uamuzi kwamba Kaunti au shirika linaweza kuuza majanichai yake moja kwa moja nje ya nchi bila kuhusisha serikali ya taifa mradi sheria ifuatwe.

Jaji Roselyne Korir wa Mahakama ya Bomet aliharamisha kifungu cha sheria za majanichai kilichosisitizia kuwa mauzo hayo lazima yafanywe kupitia mnada jijini Mombasa kabla ya kusafirishwa nje ya nchi.

Waziri wa Kilimo Peter Munya hata hivyo ametaja mauzo hayo kama feki kwa kuwa serikali ya kitaifa haikuhusishwa na pia Iran inakabiliwa na vikwazo vya kimataifa vya uchumi.

Akiwa mjini Bomet, Bw Munya alisema Bodi ya Majanichai pamoja na Mamlaka ya Kilimo cha Majanichai (KTDA) hazikuhusishwa katika majadiliano na mauzo hayo.

“Hatukuhusishwa na hata asasi mbalimbali za serikali hazikuidhinisha mauzo hayo nchini Iran. Ni Gavana Barchok pekee ambaye anaweza kutoa ufafanuzi kuhusu mauzo hayo,” akasema Bw Munya akijibu maswali wakati wa mkutano na wakulima wa kiwanda cha Kapkoros, Bomet ya Kati.

Aidha alisema kuwa viongozi wanaotaka majanichai yauzwe moja kwa moja nje ya nchi bila kupitia mnada wa Mombasa wanalenga kuwafilisi wakulima jasho lao.

“Mauzo ya moja kwa moja yatasababisha mawakala wapore wakulima pesa zao kwa kuwa hawaweki wazi bei inayotumika. Hiyo haitakuwa kwa sababu serikali pia ishaweka bei ya wastani ambayo itatumika kuuza majanichai nchini ndipo wakulima walipwe bonasi za juu,” akaongeza Bw Munya.

“Makubaliano yanayodaiwa kuwa kati ya Iran na Bomet kuhusu mauzo ya majanichai ni feki. Hakuna majanichai ambayo yamesafirishwa hadi Iran wala hayajafikishwa Mombasa ndipo yasafirisishwe nje ya nchi. Iwapo KTDA haikuhusishwa basi nani anaendesha mauzo hayo nje ya nchi?’’ akauliza Bw Munya mnamo Julai 14.

Hata hivyo, Bw Barchok alisisitiza kuwa mauzo hayo yalikuwa halali na mauzo hayo yaliendeshwa na kampuni za kibinafsi baada ya Kaunti kujaribu kuishawishi KTDA ikubali mpango huo bila mafanikio yoyote.

Kulingana na gavana huyo makubaliano na Iran yatawasaidia wakulima kupata pesa za juu na pia kuwafungulia masoko ya nje siku zijazo badala ya kutegemea serikali pekee.

You can share this post!

WABUNGE waisuta TSC kwa kubebesha walimu mzigo wa mafunzo...

Uhuru awashusha hadhi mawaziri Charles Keter na Simon...