Hatimaye Echesa atiwa nguvuni

Hatimaye Echesa atiwa nguvuni

Na SAMMY WAWERU

HATIMAYE aliyekuwa Waziri wa Michezo Bw Rashid Echesa amekamatwa kwa kumzaba kofi afisa wa Tume Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) katika uchaguzi mdogo wa ubunge Matungu, Kaunti ya Kakamga Alhamisi.

Maafisa wa polisi wamekuwa wakimsaka waziri huyo wa zamani, ambapo baada ya kugundua anatafutwa alienda mafichoni. Ijumaa, Inspekta Mkuu wa Polisi, IG Hillary Mutyambai alitoa notisi Echesa ajiwasilishe kwa idara ya polisi mara moja.

Mkuu huyo wa polisi nchini alisema endapo Bw Echesa hatajisalimisha kufikia saa saba mchana Ijumaa, “atachukuliwa kama mhalifu sugu anayemiliki silaha”.

“IG ameagiza Mheshimiwa Rashid Echesa ambaye yuko mafichoni baada ya kumdhulumu afisa wa tume ya uchaguzi ajisalimishe katika kituo chochote cha polisi kilicho karibu kufikia saa saba mchana, la sivyo atachukuliwa kama mhalifu sugu anayemiliki silaha,” taairifa ya Bw Mutyambai na iliyotolewa na Msemaji wa Idara ya Polisi, Bw Charles Owino ikaelezea.

Waziri huyo wa zamani alijisalimisha mwendo wa saa tisa alasiri katika kituo cha polisi cha Matungu, ambapo aliandamana na wakili wake.

Inaarifiwa kwamba baadaye alipelekwa katika kituo cha polisi cha Kakamega, chini ya ulinzi mkali wa maafisa wa usalama.

Kujisalimisha kwa Bw Echesa kulijiri saa chache baada ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kusema wanasiasa waliohusika katika ghasia za chaguzi ndogo Nakuru, Matungu na Kabuchai watapokonywa silaha zote zenye leseni wanazomiliki.

Dkt Matiang’i alisema serikali itahakikisha kipengele cha sita cha Katiba kimetekelezwa, ambapo wanasiasa waliohusika hawataruhusiwa kuwaninia kiti chochote cha kisiasa chaguzi za usoni.

Kwingineko, wabunge waliokamatwa eneo la Matungu kwa madai magari yao yalipatikana na silaha butu wameachiliwa na korti Ijumaa, kwa dhamana ya Sh50, 000 kila mmoja.

Mabw Nelson Koech (Belgut), Didmuss Barasa (Kimilili, Wilson Kogo (Chesumei) na seneta wa Nandi, Samson Cherargei walitiwa nguvuni Alhamisi na kukesha selini.

Kwenye video, Bw Echesa alionekana akimuangushia kofi afisa rejeshi wa tume hiyo, huku akitaka kuelezwa kwa nini maajenti wa chama cha UDA na ambacho kinahusishwa na Naibu wa Rais, Dkt William Ruto, walifukuzwa kwenye kituo kimoja cha kupigia kura.

Tukio hilo lilitendeka katika kituo cha Bulonga.

 

 

You can share this post!

Wakenya washangaa mbona Uhuru, Ruto na Raila hawajapokea...

Mpango wa kusafisha Pwani wazinduliwa