Michezo

Hatimaye Ingwe yapata mnyonge wa kunyonga

May 23rd, 2019 1 min read

NA GEOFFREY ANENE

AFC Leopards ilimaliza ukame wa mechi tano bila ushindi kwa kulipiza kisasi dhidi ya Mount Kenya United katika ushindi wao wa mabao 2-0 kwenye mechi ya Ligi Kuu ya raundi ya 32 uwanjani Kenyatta mjini Machakos, Alhamisi.

Ingwe, ambayo iliingia mchuano huu ikiuguza vichapo viliwili mfululizo kutoka kwa KCB na mabingwa Gor Mahia, ilipata mabao ya ushindi katika dakika 15 za mwisho kupitia kwa Boniface Mukhekhe. Vijana wa Casa Mbungo, ambao walilemewa na Mount Kenya 2-1 mwezi Februari, wana alama 42.

Wamerukia nafasi ya tisa na kusukuma Ulinzi Stars nafasi moja chini katika nafasi ya 10. Wanajeshi wa Ulinzi walikabwa 3-3 na Kariobangi Sharks hapo Mei 22. Mount Kenya, ambayo imeshaaga Ligi Kuu, imezoa alama 18 kwenye ligi hii ya klabu 18.

Uwanjani Ruaraka, mabingwa mara 11 Tusker walitupa uongozi mara mbili na kutoka 2-2 dhidi ya wageni wao Zoo kutoka kaunti ya Kericho.

David Majak alichenga safu ya ulinzi ya Tusker na kumwaga kipa Robert Mboya dakika ya 16. Hata hivyo, Kevin Odhiambo alihakikisha timu yake ya Zoo inaenda mapumzikoni 1-1 aliposawazisha dakika ya 36.

Mvua ilitisha kuvuruga mchuano huu wa raundi ya 32 kabla ya mapumziko. Hata hivyo, ilipungua na kuruhusu kipindi cha pili kuendelea. Mboya alijaribiwa vilivyo katika kipindi hiki pale Zoo ilimsukumia makombora kadha kabla ya Tusker kuchukua uongozi tena kupitia kwa Boniface Muchiri aliyechota frikiki safi dakika ya 72.

Tusker, ambayo ilifungwa bao la pili dakika ya 85 kutoka kwa Danson Chetambe, ina jumla ya alama 50. Inashikilia nafasi ya saba. Zoo iko katika nafasi ya 16 kwa alama 29.