Habari

Hatimaye Joho aingilia mzozo wa kusafirisha mizigo SGR

October 10th, 2019 2 min read

Na WINNIE ATIENO

GAVANA wa Mombasa, Hassan Joho sasa amejitokeza kutetea wenye biashara wanaotegemea usafirisha mizigo kwa malori kutoka Bandari ya Mombasa.

Hii ni baada yake hapo Jumatano kutishia kuongoza maandamamo makubwa endapo serikali haitaruhusu malori kubeba kontena kutoka bandari ya Mombasa kama ilivyoahidi wiki jana.

Uchumi wa Mombasa unategemea bandari na utalii na kwa muda sasa wafanyabiashara wamekuwa wakishutumu agizo kuwa makasha yote kutoka bandari hiyo yasafirishwe kwa reli ya SGR pekee.

“Watu wameongea mambo ya SGR lakini mimi nikasema njia ni mazungumzo. Mimi ni mtu wa heshima lakini sishindwi kuingia barabarani… na nitaingia kwa kishindo,” alisema Bw Joho.

Akiongea kwenye hafla ya uzinduzi wa malori ya kuzoa taka katika eneo la Treasury Square, Bw Joho alisema ataitisha maandamano iwapo mbinu zingine zitakosa kufanikiwa.

Kwa kipindi cha mwezi mmoja sasa, wafanyabiashara mjini Mombasa wamekuwa wakiandamana kila Jumatatu baada ya kuzuiwa kuchukua mizigo bandarini licha ya agizo la serikali kuwaruhusu wiki iliyopita.

Waziri wa Uchukuzi James Macharia na mwenzake wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i waliiamuru Halmashauri ya Bandari nchini (KPA) iruhusu mizigo kuchukuliwa kwa trela iwapo waagizaji wanataka hivyo.

Wafanyabiashara hao walisema KPA iliwakataza kuingia bandarini wiki jana kwa madai kuwa haijapata agizo kutoka kwa mawaziri hao.

Katika mkutano wa washikadau uliohudhuriwa pia na viongozi mbalimbali wakiwemo Seneta Mohammed Faki na Mbunge wa Kisauni Ali Mbogo, wahusika walilalamikia kuzimiwa biashara.

Katika mkutano huo, Bw Mbogo alifurushwa alipotofautiana na wafanyabiashara hao baada ya kutoa kauli zilizokuwa zikisifu Bw Macharia na Rais Uhuru Kenyatta.

Mwezi uliopita, ripoti ya utafiti iliyotolewa na Chuo Kikuu cha Nairobi (UoN) na kukabidhiwa Gavana Joho na viongozi wengine kutoka Pwani, ilionyesha hali ya uchumi Pwani inazidi kuzorota tangu SGR ilipozinduliwa.

Katika ripoti hiyo, asilimia 60 ya wafanyakazi waliokuwa wakifanya kazi katika mabohari ya mizigo (CFS) wamefutwa kazi, huku madereva wa matrela wakiathirika pia.

Takwimu zilionyesha kuwa wafanyakazi 2,987 katika sekta mbalimbali walipoteza kazi kwa muda wa mwaka mmoja uliopita.