Habari Mseto

Hatimaye Joho aonekana hadharani kwenye harusi ya Ali Kiba

April 19th, 2018 2 min read

Na MOHAMED AHMED

BAADA ya kukosa kuonekana hadharani kwa takriban miezi mitatu, Gavana wa Mombasa Hassan Joho hatimaye alionekana kwa mara kwanza Alhamisi katika harusi ya msanii wa Bongo, Ali Saleh almaarufu Ali Kiba.

Wakati wa harusi hiyo iliyofanyika katika msikiti wa Ummul Kulthum eneo la Kizingo, Bw Joho alionekana kuepuka hadhira na kuingia msikitini humo kwa siri akitumia mlango wa nyuma.

Bw Joho alikuwa nchini Estonia na baadaye alienda Uhispania kwa safari za kikazi, kulingana na usimamizi wa afisi yake.

Taifa Leo iliyokuwa imekita kambi msikitini hapo kwa ajili ya harusi ya Kiba ilimuona Bw Joho akiingia na gari jeupe bila ya kuandamana na walinzi wake.

Waandishi wa habari walizuiliwa kupiga picha katika harusi hiyo ambayo ilikuwa inapeperushwa na Azam TV ya Tanzania.

Baada ya harusi kufungwa, gavana huyo ambaye pia ni naibu kiongozi wa chama cha ODM alitoka hivyo hivyo kwa siri akiepuka kunaswa na kamera za waandishi waliokuwa hapo.

Licha ya harusi hiyo kufanywa kisiri asubuhi mapema jana, harusi hiyo iling’oa nanga kwa shwange kubwa Mombasa.

Ali Kiba aliyekuwa ameandamana na nduguye Abdu Kiba walifika katika msikiti huo ambao ujenzi wake ulisimamiwa na familia ya Joho mapema kwa ajili ya sherehe hiyo ya Nikkah.

Baada ya aya chache za Korani kusomwa muda ukawadia na Sheikh Mohammed Kagera akashika kiganja cha Kiba kumuozesha mchumba wake Amina Khalef.

Kiba akafuatisha: “Mimi Ali Saleh nimekubali kumuoa Amina Khalef kwa mahari tuliosikizana na ikitokea sababu ya kuachana tuachane kwa wema.”

Tabasamu lake la kawaida likaja kinywani mwake baada ya kuitika mwito huo. Kiba alikuwa amevalia gauni linalotambulika kama joho na kilemba na kushika upanga kama ilivyo desturi ya tamaduni ya Uswahilini.

Katika mahojiano mafupi Kiba alisema: “Nafurahi siku yangu imewadia. Sina mengi ya kusema kwa sasa,” akasema kabla gari alilokuwa ndani kuondoka.

Baada ya kutoka msikitini waalikwa walienda nyumbani kwa nduguye Joho, Abu Joho eneo la Kizingo kwa ajili ya kula bembe la harusi.

Bwanahurusi kisha alifululiza mpaka kwa kina bibi harusi eneo la Kongowea kumuona mkewe kama ilivyo ada.

Baadaye mlo wa waalikwa pekee uliandaliwa eneo hilo la Kizingo na baadae Joho akaandamana na Kiba katika jumba lake la Vipingo, kaunti ya Kilifi.

Alhamisi jioni wanawake walikusanyika katika ukumbi wa Diamond Jubilee kwa sherehe ya kupamba ambapo bibi harusi aliingia kwa madaha na waalikwa waliokuwa na hamu kumuona kichuna huyo.