Habari Mseto

Hatimaye meli ya mwaka 2020 yang'oa nanga

January 1st, 2020 2 min read

Na KALUME KAZUNGU na SAMMY WAWERU

WAKENYA na wageni wa tabaka mbalimbali wameukaribisha mwaka mpya kwa mbwembwe shughuli nyingi zikiwa ni Pwani ya Kenya na jijini Nairobi.

Katika Kaunti ya Lamu, wageni na watalii mbalimbali waliukaribisha mwaka mpya wa 2020 kwa mtindo wa aina yake, ambapo wengi walionekana wakijivinjari ndani ya bahari.

Boti na mashua mbalimbali zilizojaa wakazi na watalii zilionekana zikizunguka baharini ilhali nyingine zikiwa zimetia nanga katikati ya bahari huku zikiwa zimepambwa kwa mataa ya rangi tofautitofauti, hivyo kuleta mvuto wa aina yake.

Wapenda raha wengine pia waliukaribisha mwaka mpya kwa kumiminika kwenye baa ya aina ya boti inayoelea kwenye Bahari Hindi, kati ya mji wa kale wa Lamu na Shella-almaarufu Floating Bar.

Baadhi ya waliohojiwa hawakuficha furaha yao kwa kufanikiwa kuvuka mwaka wakiwa hai.

Bw William Romano, mtalii kutoka Uhispania alimshukuru Maulana kwa kumuajalia afya bora.

“Ni furaha yangu kwamba Mungu ametukirimu afya na uhai. Nimesafiri kutoka Uhispania hadi Lamu ili kujumuika na wakenya hapa kuukaribisha mwaka 2020. Nawatakia nyote Mwaka Mpya wenye fanaka,” akasema Bw Romano.

Bi Judith Mwangi alisema aliamua kuukaribisha mwaka mpya akiwa eneo la Floating Bar kama kawaida yake kila mwaka.

Alisema anapenda eneo hilo ambalo ni tulivu, akisisitiza kuwa humwezesha kutafakari mipango anayopania kufanya kila mwaka mpya unapowadia.

“Hapa hakuna fujo. Ni raha tupu. Napenda hapa. Hutatrizwi na yeyote wakati unapokaribisha mwaka mpya wako. Tuzidi kumuomba Mungu atupe neema ili mwaka 2020 uwe wa mafanikio,” akasema Bi Mwangi.

Wale waliokuwa wameabiri boti na mashua baharini walisikika wakiimba na kucheza nyimbo za kutukuza Mwaka Mpya.

Wengine pia walichukua fursa hiyo kubugia pombe ilmradi wakaribishe mwaka mpya kwa mtindo wanaotaka wao.

Jijini Nairobi

Jijini Nairobi, kuna waliojumuika katika maeneo ya kuabudu, burudani na hata katika baa kuukaribisha mwaka huu wa 2020 ambao kalenda yake imeng’oa nanga hii leo Jumatano, Januari 1.

Sawa na miji mingine mikuu ulimwenguni, ilipotimia saa sita usiku (0000Hrs) anga ya jiji la Nairobi ilisheheni miako ya fataki, ishara kuwa mwaka 2019 umekamilika na kulaki 2020.

Mitaa iliyoko karibu na Thika Superhighway, kama vile Kasarani, Zimmerman, Mwiki, Githurai, Kahawa West na mingineyo, kwa muda wa takriban dakika kumi anga yake ilihinikiza fataki zilizorushwa na wananchi waliofurahia kuona mwaka mpya.

“Huu ni mwaka wa aina yake, kinyume na miaka mingine fataki tulizoshuhudia mwaka huu ni nyingi,” akasema mkazi mmoja wa mtaa wa Zimmerman na ambaye alikaribisha 2020 katika mazingira anayoishi.

Mbali na waliojumuika na wenzao maeneo mbalimbali na katika mazingira wanayoishi, magari kadha yalionekana yakisafiri Thika Super Highway.

Kwa kawaida, katika mitandao ya kijamii kama vile Facebook, Instagram, Twitter na Whats App, wengi walipakia jumbe za heri njema. “Tunapokaribisha 2020, ninawatakia mema na ufanisi. Ikiwa hukufanikisha mikakati yako 2019, usiratibu mipya 2020. Hakikisha uliyoanza imetimia, kabla kuorodhesha mingine. Muhimu zaidi ni kumhusisha Mwenyezi Mungu kwa maombi,” akachapisha Charles Gathogo.

Kwenye salamu zake za heri njema, Rais Uhuru Kenyatta alihimiza umuhimu wa umoja na amani ili kuafikia malengo ya maendeleo. “Kama Rais, nitaendelea kuimarisha mazingira ya umoja. Tuweke kando tofauti za kisiasa tuungane ili kukuza taifa,” akasema kiongozi huyo wa taifa.

Rais Kenyatta pia alitaja ripoti ya Jopo la Maridhiano (BBI), iliyobuniwa 2018 kupitia salamu za maridhiano kati yake na kiongozi wa ODM Raila Odinga, ajenda kuu nne, kuendeleza vita dhidi ya ufisadi, miongoni mwa vigezo vingine, kama anayopania kuafikia.