Michezo

Hatimaye Mieno atua St Georges, Ethiopia

January 15th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

KIUNGO wa Gor Mahia Humphrey Mieno hatimaye amejiunga rasmi na vigogo wa soka wa nchi jirani ya Ethiopia, St Georges FC.

Mieno ambaye pia aliwahi kusakatia mabingwa wa zamani Tusker na Sofapaka, Jumatatu Januari 14 alimwaga wino kwenye mkataba wa miaka miwili baada ya maafisa wa K’Ogalo na wenzao wa St Georges kuafikiana wakiwa wameshiriki mwezi moja wa majadiliano ya kina.

Mwanadimba huyo pia alitia saini makubaliano ya kibinafsi na maafisa wa klabu hiyo waliosafiri kwa ndege hadi jijini Nairobi kukamilisha uhamisho huo. Hata hivyo kiwango cha hela atakachotia mfukoni  Mieno kila mwezi hakikuwekwa wazi japo inadaiwa kwamba atalipwa nyongeza ya mshahara wa asilimia 100 kuliko ule alikuwa akipata akiwa Gor Mahia.

Vile kuna fununu kwamba usajili huo huenda uligharimu Sh6milioni ingawa uongozi wa klabu zote haujajitokeza kukanusha wala kukubali fununu hizo.

“Ni kweli kwamba uhamisho wake sasa ni rasmi baada ya pande zote kuafikiana. Mieno sasa yu huru kujiunga na St Georges kwa kandarasu ya miaka miwili,” akasema afisa moja wa Gor Mahia ambaye hakutaka jina lake linukuliwe kwa kuwa haruhusiwi kuzungumza kwa niaba ya klabu.

Mieno hajakuwa akishirikishwa katika michuano ya ligi ya Gor Mahia na ilidaiwa alikuwa amegomea timu hiyo kama njia ya kuishurutisha kukamilisha uhamisho wake.

Mwanasoka huyo sasa atajiunga na mnyakaji mahiri wa timu ya taifa Harambee Stars Patrick Matasi anayenyakia timu hiyo na kocha wa zamani wa Sofapaka Steward Hall ambaye pia alikuwa mkufunzi wa Mieno akisakatia Batoto ba Mungu.