Kimataifa

Hatimaye mitishamba ya Covid-19 yatua TZ

May 10th, 2020 1 min read

Na MASHIRIKA

ANTANANARIVO, MADAGASCAR

TANZANIA hatimaye imepokea dawa ya mitishamba inayosemekana kutibu wanaougua Covid-19 kutoka kwa Serikali ya Madagascar.

Akipokea dawa hiyo Ijumaa nchini Madagascar, Waziri wa Mashauri ya Kigeni Tanzania, Prof Palamagamba John Kabudi alikanusha madai kwamba Tanzania ililegea katika kupambana na janga la corona.

Kwa upande wake, Waziri wa Mambo ya Nje wa Madagascar Tehindrazanarivelo Djacoba As Oliva alitoa wito kwa nchi za Afrika kuungana kwa pamoja kupata suluhisho la maradhi ya Covid-19.

Mnamo Mei 3, 2020, Rais wa Tanzania John Pombe Magufuli aliahidi kutuma ndege Madagascar kwenda kufuata dawa hiyo ya mitishamba.

Wakati huo Dkt Magufuli alisema kuwa amewasiliana na Madagascar baada ya kupokea barua rasmi kutoka nchi hiyo iliyoeleza kuwa wamegundua dawa ya corona.

Shirika la Afya Duniani (WHO) lilisema ni muhimu dawa zinazosemekana kuwa na uwezo wa kutibu zifanyiwe majaribio kwanza.

Shirika hilo lilionya huenda watu wakaona wamepata tiba na kujihisi kuwa salama ilhali wametumia dawa ambazo hazijafanyiwa majaribio.

Wakati huo huo, serikali ya Tanzania ilijitetea kwa kusitisha matangazo kuhusu hali ya corona nchini humo kwa takriban wiki moja sasa.

Matangazo hayo yalisitishwa baada ya Dkt Magufuli kutilia shaka shughuli za maabara makuu yaliyotegemewa kupima virusi hivyo.

Kulingana na Magufuli, kulikuwa na shaka kwa vile serikali ilituma sampuli za vitu tofauti kama vile papai na mbuzi, kisha ripoti zikatolewa kutoka kwa maabara kwamba sampuli hizo zilikuwa na virusi vya corona.

Waziri wa Afya nchini Tanzania, Ummy Mwalimu alisema kimya cha serikali kuhusu maambukizi kilitokana na hatua zinazoendelezwa kuboresha maabara ya taifa.

“Kama mnavyofahamu kuna kazi za kiufundi zinazoendelea kwa hivyo nataka niwaondolee watu hofu tu kwamba ndani ya siku chache kazi itakuwa imekamilika na hivyo tutaendelea kutoa taarifa kwa umma mara kwa mara,” akasema.