Hatimaye msimu mpya wa EPL waanza leo

Hatimaye msimu mpya wa EPL waanza leo

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

MSIMU mpya wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) 2021/2022 utaanza rasmi leo usiku kwa mechi moja kati ya vigogo wa Arsenal dhidi ya Brentford waliopanda majuzi.

Ligi hiyo inayojumuisha timu 20 itaendelea kesho na Jumapili katika viwanja mbalimbali ambapo mashabiki watashuhudia timu zao zikiwachezesha wachezaji kadhaa wapya.

Kocha Mikel Arteta ameeleza jinsi alivyokabiliwa na wakati mgumu kupata wachezaji wapya, katika juhudi za kuhakikisha kikosi kipo imara, hata baada ya timu yake kulemewa katika mechi za maandalizi na kuandikisha ushindi pekee dhidi ya Watford na Millwall.

Ni mechi ambayo watatakiwa kucheza kwa makini ikikumbukwa kwamba kikosi cha Brentford chini ya kocha Thomas Frank kina washambuliaji matata wakiongozwa na Ivan Toney aliyefunga mabao 31 katika ligi ya Daraja la Kwanza msimu uliopita.

Brentford wanaingia uwanjani baada ya kuandikisha ushindi wa 2-1 dhidi ya Valencia katika mechi ya kupimana nguvu, matokeo ambayo yanawapa matumaini makubwa.

Hii itakuwa mara ya kwanza kwa klabu hiyo kucheza mechi za EPL tangu 1947.

Ushindi utakuwa mwanzo mzuri kwa Arsenal ambao watakutana na Chelsea kabla ya kuvaana na Manchester City kwenye mechi zitakazofuata.

Baada ya kumaliza ligi katika nafasi ya nane na kukosa kufuzu kwa michuano ya Klabu Bingwa, Arsenal wanahitaji ushindi kwa vyovyote vile ili kuwapa mashabiki wao matumaini.

Emile Simth Rowe na Bukayo Saka wanatarajiwa kuongoza safu ya mashambuliaji, baada ya majuzi kushindwa kuwika katika mechi za maandalizi.

Pierre-Emerick Aubameyang alionyesha kiwango duni kwenye mechi hizo, lakini huenda akapata nafasi kikosi, wakati Arteta anatarajiwa kuanzisha kikosi kilichopimana nguvu na Tottenham Hotspur.

Safu ya ulinzi inatarajiwa kuwa chini ya Albert Sambi Lokonga akisaidiana na Grant Xhaka, huku Emile Smith Rowe akiongoza mashambuliaji.

Manchester United ambayo ni miongoni mwa timu tajiri zaidi kwenye ligi hiyo itakuwa nyumbani kesho alasiri kuvaana na Leeds United, wakati mabingwa wa Ulaya Chelsea wakiialika Crystal Palace ugani Stamford Bridge katika pambano jingine baadaye.

Mabingwa wa sasa, Manchester City watasubiri hadi Jumapili kupepetana na Tottenham Hotspur ugenini.

“Tulikuwa na lengo la kusajili wachezaji kadhaa kabla ya msimu kuanza, lakini hali mbaya ya kiuchumi imetuvuruga. Hata hivyo, kikosi cha kutegemea kipo na pia tunafurahia kumpata Ben White miongoni mwa wachache tuliofanikiwa kusajili,” alisema Mhispania huyo.

Ratiba kwa ufupi:

Leo Ijumaa: Brentford na Arsenal.

Kesho (Jumamosi): Manchester United na Leeds United, Leicester City na Wolves, Chelsea na Crystal Palace, Watford na Astona Villa, Everton na Southampton, Burnley na Brighton, Norwich City na Liverpool.

Jumapili: Newcastle United na West Ham.

You can share this post!

Visa vya wizi wa pikipiki za bodaboda vyaongezeka Witeithie

Corona yaponda miji na vijiji