Habari

Hatimaye Mugo wa Wairimu abambwa

November 13th, 2018 1 min read

Na CHARLES WASONGA

DAKTARI bandia James Mugo Ndicho maarufu kama Mugo wa Wairimu alikamatwa Jumanne jioni katika  eneo la Gachie, kaunti ya Kiambu baada ya kusakwa na polisi kwa majuma mawili.

Mugo alikamatwa na maafisa wa kikosi cha Flying Squad ambao walikuwa wakimwandama mchana kutwa. Alikuwa amejificha katika nyumba ya binamu yake polisi walipomfumania mwendo wa saa moja usiku.

“Atakabiliwa na mkono wa sheria inavyohitaji,” mkuu wa Flying Squad Bw Bernard Yego akaambia polisi.

Mugo amekuwa akikwepa mtego wa polisi tangu Novemba 3 habari zilipomfikia kwamba wafanyakazi wake walitiwa mbaroni jijini Nairobi.

Wafanyakazi hao, ambao  walisemekana kuwa wahudumu wa afya wameshtakiwa mahakamani.

Maafisa wa polisi ambao wamekuwa wakimsaka Mugo walisema kuwa alikuwa akitumia kadi 15 tofauti za simu kuwasiliana na watu tofauti huku akizunguka kutoka pahali moja hadi pengine.

Wakati mmoja ilibainika kuwa alionekana katika maeneo ya Makuyu, Thika, Kiambu na baadaye Gachie.

Bw Yego alisema kuwa watamhoji daktari huyo feki kabla ya kumwasilisha mahakamani Jumatano.

Mugo anakabiliwa na tuhuma ya kumdhulumu kimapenza mgonjwa baada ya kumpa dawa ya kumfanya apoteze fahamu, kitendo ambacho inasemekemana amekuwa akitekeleza katika kliniki ya kwa muda mrefu.

Vile vile, anadaiwa kuendesha kliniki bandia katika mtaa wa Kayole jijini Nairobi.

Wafanyakazi wake wawili, ambao walikuwa wakihudumu bila stakabadhi halali, walikamatwa katika operesheni iliyoendeshwa na polisi baada ya Bodi ya Madaktari na Wataalamu wa Meno kuwasilisha malalamishi.

Maafisa hao wa polisi ambao waliandamana na Afisa Mkuu Mtendaji wa bodi hiyo Daniel Yumbia, alipata vifaa ambavyo viliaminika kutumia kuwasaidia wanawake kuavya mimba katika kliniki hiyo.