Michezo

Hatimaye ndovu Cote d’Ivoire wapanda mtini

January 30th, 2024 2 min read

NA MASHIRIKA

WENYEJI, Cote d’Ivoire wamefuzu kwa robo-fainali ya Kombe la Taifa Bingwa Afrika (Afcon 2023) baada ya kubandua mabingwa watetezi Senegal 5-4 kupitia kwa mikwaju ya penalti katika pambano la hatua ya 16-bora.

Hii ni baada ya mechi iliyochezwa Jumatatu usiku kumalizika kwa sare ya 1-1 hata baada ya muda wa ziada katika uwanja wa Stade Charles Konan Banny, na sasa watakutana na mshindi kati ya Mali na Burkina Faso ambao wamepangiwa kukutana Jumanne usiku.

Senegal almaarufu ‘Lions of Teranga’ walitangulia kufunga bao kupitia kwa Habib Diallo kabla ya Franck Kessie kusawazisha dakika chache kabla ya mechi hiyo kumalizika katika muda wa kawaida wa dakika 90.

Baada ya kupuuzwa na kupangwa katika kikosi cha akiba, Kessie aliyeingia dakika ya 73 katika nafasi ya Sangare aliwafungia penalti ya kusawazisha dakika ya 86 kabla ya kupachika wavuni nyingine ya ushindi katika muda wa ziada.

Wenyeji walipewa penalti baada ya kipa Edouard Mendy kumuangusha kijisandukuni Nicolas Pepe aliyekuwa akielekea langoni kufunga bao.

Mbali na kumpa nafasi nyota huyo mzoefu, kocha Emerse Fae aliyeteuliwa kuchukua nafasi ya Jean-Louis Gasset vile vile alifanya mabadiliko mengine kwa kuwaleta Christian Kouame, Sebastian Haller, Nocolas Pepe katika nafasi za Odilon Kossounou, Seko Fofana, Omar Diakite, na Max Gradel, mabadiliko ambayo yalipandisha presha mabeki wa Senegal.

Kessie alifunga bao la kusawazisha muda mfupi tu baada ya Sadio Mane kukosa nafasi nzuri katika eneo la hatari.

Awali katika mechi za makundi, Cote d’Ivoire walikumbana na matokeo ya kushtusha, kikiwemo kichapo cha 4-0 kutoka kwa Equatorial Guinea na kufuzu kwa 16-Bora kwa sheria ya timu tatu bora.

Mashabiki wao walichukizwa na wachezaji baada ya kipigo hicho na ikabidi wazuiliwe kutoka uwanjani kwa sababu za kiusalama.

Lakini Jumatatu, kikosi hicho kilifufuka na kuwa matata zaidi huku kocha Fae akiwa na matumaini kwamba sasa kina nafasi kubwa ya kutwaa ubingwa.

“Tulitatizika hapo awali, lakini tutakuwa makini zaidi katika mechi ijayo baada ya kufuzu kwa bahati. Ningependa kuwahakikishia mashabiki kwamba tumegundua shida yetu na tutazidi kuwafurahisha. Lazima tucheze vizuri na kutumia nafasi zitakazopatikana vyema, kwani tukilegea, zinaweza kutugharimu,” akasema kocha Fae.

Kwa upande mwingine, kocha Aliou Cisse wa Senegal amekiri kwamba wenyeji walikuwa wazuri katika mechi hiyo iliyohudhuriwa na zaidi ya mashabiki 20,000.

“Nakubali wenzetu walikuwa bora kutuzidi. Walimiliki mpira kwa kiasi kikubwa na kutengeneza nafasi nyingi. Walikuwa kila mahali, hasa walipoingiza wachezaji kadhaa walio na ujuzi mwingi,” alikiri Cisse ambaye alikuwa kiungo mahiri alipochezea timu hiyo zaidi ya miaka 14 iliyopita.