HabariSiasa

Hatimaye Raila atazama mwili wa Moi

February 10th, 2020 3 min read

Na CHARLES WASONGA

KIONGOZI wa ODM Raila Odinga Jumatatu aliungana na Wakenya kutoa heshima zake za mwisho kwa Rais wa zamani marehemu Daniel Arap Moi katika majengo ya bunge, Nairobi.

Waziri huyo Mkuu wa zamani aliwasili katika majengo hayo mwendo wa saa nane na nusu alasiri akiwa ameandamana na mkewe Ida na mwanawe Raila Junior.

Bw Odinga alionekana kuinua mgwisho (fly-whisk) aliyopewa na Raila Junior mara tatu kabla ya kuinama kwa heshima na Mzee Moi aliyemtaja kama “mpiganiaji uhuru na kiongozi mcheshi aliyependa watu.”

Bw Odinga alifika katika majengo ya bunge saa chache baada ya kuwasili kutoka nchini Ethiopia ambako alihudhuria mkutano wa viongozi wa nchini wanachama wa Muungano wa Afrika (AU) jijini Addis Ababa.

Kwenye mkutano mfupi ya wanawe marehemu Moi, Raymond na Gideon, Bw Odinga alielezea namna ambayo mwendazake alishirikiana na babake Jaramogi Oginga Odinga kupigania uhuru wa Kenya.

“Mzee alikuwa mpiganiaji uhuru shupavu. Yeye pamoja na babangu walikuwa miongoni mwa Wakenya wa kwanza kuchaguliwa kama wajumbe katika Bunge la Kenya (Legco) mnamo 1957,” akasema.

Wengi walikuwa wametarajia kwamba Bw Odinga angefika kwenye majengo hayo na kumwomboleza Mzee Moi kulingana na tamaduni za jamii ya Waluo maarufu kama ‘Tero Buru’ lakini hilo halikufanyika.

Mnamo 2003, Bw Odinga alimwomboleza aliyekuwa Makamu wa Rais Kijana Wamalwa akiwa amevalia mavazi ya kitamaduni na kushika mkuki mkononi jinsi Waluo huomboleza watu mashuhuri walioaga dunia.

Baada ya kumaliza kuutazama mwili wa Mzee Moi, Waziri huyo Mkuu wa zamani alielekea kwenye chumba cha pembeni na kukutana na familia ya Mzee Moi wakiongozwa na seneta wa Baringo Gideon Moi na mbunge wa Rongai Raymond Moi.

Wawili hao walimwaarifu kuhusu mipango ya mazishi na kumwalika rasmi afike Nyayo leo na Kabarak kesho kwa mazishi.

“Tutakuwa na ibada Jumanne katika uwanja wa Nyayo na kesho Kabarak ambazo zitaanza saa tatu. Tunataka kumaliza mapema kisha tuwaruhusu watu warudi makwao kwa sababu wengi watafika na baadhi wanatoka maeneo ya mbali,” Gideon Moi akamweleza.

Bw Odinga naye alikubali wito wa kufika kwenye ibada hizo na akaeleza historia fupi kati ya familia ya babake marehemu Oginga Odinga na Mzee Moi kabla na baada ya uhuru.

“Kwa niaba ya familia ya marehemu Jaramogi Oginga Odinga na familia yangu tutafikisha rambirambi. Mzee alikuwa mpiganiaja na yeye na marehemu babangu walikuwa watu wa kwanza kuchaguliwa kwenye Bunge la Legco. Nimemjua tangu 1958. Leo ni siku ya kufikisha rambirambi zetu na nilipokea habari za kifo chake nikiwa na Rais Uhuru Kenyatta Marekani,” akasema.

“Nikiwa Addis Ababa niliwafahamisha Marais wa mataifa mbalimbali kuhusu tanzia hii na wameahidi kufika hapa kesho kwa mazishi. Mzee ameishi maisha kamilifu na Mungu ailaze roho yake mahala pema peponi,” akaongeza Bw Odinga.

Familia hiyo kisha ilimshukuru pamoja na Wakenya wengine kwa kuomboleza nao.

‘Tungependa kukushukuru kwa kufika na kukubali kuwa nasi kesho Nyayo na Kabarak. Tunakukaribisha na zaidi ya raia 200,000 ambao wamefika hapa kuona mwili wa Mzee Moi,” akasema Raymondi Moi.

Waziri huyo mkuu wa zamani aliwasili kutoka Addis Ababa Ethiopia Jumapili usiku ambako aliwakilisha Rais Kenyatta katika mkutano wa Muungano wa Afrika (AU) uliokamilika hapo jana.

Kando na Bw Odinga, maelfu ya Wakenya jana walifika majengo ya bunge kutazama mwili huo siku ya mwisho.

Mlolongo mrefu wa raia ulianza katika jumba la Kencom, ukapitia karibu na Mahakama ya Juu hadi majengo ya Bunge huku usalama ukiimarishwa na polisi na vijana wa NYS.

Baadhi ya raia waliokuwa kwenye foleni walilemewa na kuzirai kutokana na wakapewa huduma za kwanza na vijana wa NYS pamoja na wasamaria wema.

Wengi walivumilia miale mikali ya jua ili kuona mwili huo ambao umekuwa katika majengo ya bunge tangu siku ya Jumamosi.

Shughuli hizo zilikamilika saa 11 na mwili huo kurejeshwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Lee huku ibada ikitarajiwa kuandaliwa leo katika uwanja wa Nyayo na kuongozwa na madhehebu mbalimbali.

Rais Uhuru Kenyatta, Naibu wake William Ruto na Bw Odinga, viongozi mbalimbali na maafisa wa ngazi za juu wanatarajiwa kuhudhuria ibada ya leo na mazishi siku ya kesho.

Itakumbukwa kuwa Bw Odinga ni miongoni mwa wanasiasa na wanaharakati ambao walifungiwa katika vyumba vya mateso katika yaliyokuwepo katika jumba la Nyayo House, wakati wa utawala wa Moi. Alitupwa kizuizini kwa miaka minane kwa kuhusishwa na jaribio la mapinduzi ya serikali mnamo 1982.

Hata hivyo, katika risala zake za rambirambi wiki jana, Bw Odinga alisema kuwa amemsamehe Moi kwa mateso aliyopitia chini ya utawala wake.

Kabla ya kumpokeza Mwai Kibaki mnamo 2002, Mzee Moi aliomba msamaha hadharani kutoka kwa wale wote ambao huenda aliwakosea kwa njia moja ama nyingi wakati wa utawala wake wa miaka 24.