Hatimaye Ruto apokea chanjo ya corona

Hatimaye Ruto apokea chanjo ya corona

Na SAMMY WAWERU

NAIBU wa Rais Dkt William Ruto na mke wake, Mama Rachael Ruto Jumanne walijiunga na orodha ya viongozi wakuu serikalini waliopokea chanjo ya Covid-19.

Wawili hao, walipata chanjo hiyo katika makazi yao Karen, jijini Nairobi.

“Chanjo ya Covid-19 ni ‘chombo’ salama kuzuia maisha yetu na kukabili ugonjwa huu. Ninahimiza Wakenya kushiriki katika zoezi hili ili tujilinde dhidi ya janga hili na kuzuia maenezi zaidi,” akachapisha Dkt Ruto katika kurasa zake za mitandao ya kijamii, chapisho lililoandamana na picha zake na mke wake, Mama Rachael wakidungwa.

“Mimi na familia yangu tumepokea chanjo ya Covid-19, Karen, Nairobi,” akaelezea Naibu wa Rais.

Dkt Ruto amejiunga na orodha ya baadhi ya viongozi wakuu serikalini waliopata chanjo ya virusi vya corona.

Mwishoni mwa juma lililopita Rais Uhuru Kenyatta na mke wake na ambaye ni Mama wa Taifa, Bi Margaret Kenyatta walipokea chanjo.

Mawaziri, Dkt Fred Matiang’i (Usalama wa Ndani na Mikakati ya Serikali) na Mutahi Kagwe (Afya) pia walipokea chanjo hiyo pamoja na Rais, katika hafla iliyoandaliwa Ikulu ya Nairobi, baada ya kiongozi huyo wa nchi kuhutubia taifa Ijumaa, Machi 26, 2021.

Maafisa wengine wakuu serikalini, wakiwemo magavana na viongozi wa kidini pia walipata chanjo hiyo ya AstraZeneca na inayoendelea kutolewa kote nchini.

Wahudumu wa afya, maafisa wa usalama na walimu ndio walitangulia.

Serikali pia imejumuisha wazee waliofikisha umri wa miaka 58 na zaidi.

You can share this post!

Nike yafika mahakamani kushtaki kampuni kuhusu ‘viatu...

Kilio Kaunti ya Mombasa kuamuru wakazi watumie daraja jipya...