Hatimaye Samsung Galaxy S21 Ultra yaingia katika soko la Kenya

Hatimaye Samsung Galaxy S21 Ultra yaingia katika soko la Kenya

NA RICHARD MAOSI

BAADA ya kutangaza kutamatika kwa kutengenezwa kwa simu aina ya Galaxy S21 hapo Januari, kampuni ya Samsung Ijumaa imezindua rasmi simu hizo katika soko la Afrika Mashariki, katika mkahawa wa Urban Eatery jijini Nairobi.

Wakenya wengi walioisubiria kwa hamu simu aina ya Galaxy S21 Ultra, sasa wanaweza kuinunua katika maduka ya Samsung jijini Nairobi kwa bei ya Sh170,000.

Hafla yenyewe ililenga kuonyesha namna ubunifu umesaidia kuunda mifumo ya kisasa ya vifaa, na kusaidia kuwapa watumizi simu za teknolojia ya hali ya juu zaidi, ambazo wamekuwa wakiagiza.

Samsung ilitumia fursa hiyo pia kuzindua simu aina ya A Series,  kwa lengo la kuwafikia mamilioni ya Wakenya ambao hutumia simu za bei nafuu.

“Simu ya A12 itauzwa kwa Sh18,500, ya A122 Sh15,000. Aina hii ya mifumo ya simu itauzwa kwa kati ya Sh11,000 na Sh50,000,” ilisema kampuni hiyo.

Baadhi ya wateja wakikagua aina mbalimbali za simu za kisasa zilizozinduliwa na Samsung Ijumaa, jijini Nairobi. Picha/ Richard Maosi

Bw Charles Kimari, Mkuu wa Mauzo ya Samsung Afrika Mashariki aliambia Taifa Leo Dijitali kuwa watumiaji wa kila rika wanaendelea kufurahia huduma zake.

“Lengo kuu ni kuhakikisha wateja wetu wanarahisisha mawasiliano, kufanya biashara na kutangamana kwenye kumbi mbalimbali,” akasema.

 

Maelezo ya kina kuhusu simu hizo yalitolewa, kwa lengo la kumwezesha mnunuzi ajipatie simu itakayomfaa kulingana na mahitaji yake..

Miundo ya Galaxy S21 ilianza kuitishwa na wateja kabla ya kuzinduliwa, mara ya kwanza wakipiga oda hapo Januari 22 na kuendelea kuiagiza hadi Februari 11, 2021.

Charles Kimari anayesimamia mauzo ya Samsung Afrika Mashariki akiwa na afisa mwenzake Chandn Verma wwakifurahia picha ya pamoja baada ya kuzindua Galaxy S21 jijini Nairobi Ijumaa. Picha/Richard Maosi

“Mwaka wa 2021 umekuja na ari mpya, kwa sababu tumegundua wateja wengi wamekuwa wakinunua simu za kisasa,” aliongezea Bw Kimari.

Alieleza kuwa ununuzi wa simu za kisasa, uliongezeka kwa zaidi ya asilimia 30, jambo lililofanya watengenezaji kubadili mitindo ya mauzo.

Kulingana naye mwaka wa 2020, umekuwa tofauti na 2021 kwa mambo mengi kama vile, rangi za simu ambazo wateja wamekuwa wakinunua.

Simu aina ya Samsung A02s iliyozinduliwa Ijumaa inauzwa kwa Sh14,500. Picha/ Hisani

Kwa mfano mwaka uliopita wanaume wengi walinunua simu nyeusi, huku akinadada wakinunua simu za rangi mbalimbali kama vile hudhurungi na kahawia.

“Mwaka uliopita tulishuhudia idadi kubwa ya watumiaji wakionekana kupendelea aina ya simu za punde zaidi, mojawapo ikiwa ni ile ya A51, ambayo iliongoza kwa mauzo kote ulimwenguni,” alisema.

Muundo wa Galaxy S21 unaundwa na daftari na kalamu ya kidijitali. Isitoshe teknolojia yake inafanikisha kuchora, kuandika , kuhariri na kupiga picha kutoka mbali.

Afisa wa Samsung akimwonyesha mteja jinsi ya kutumia simu mpya ya Samsung Galaxy S21. Picha/ Richard Maosi

Kalamu hiyo ambayo imewiana na muundo wa simu itamwezesha mtumiaji kuhariri makala ya video mpaka hatua ya mwisho bila kupoteza ubora.

Teknolojia hii ikionekana kupendwa na watumizi ikilinganishwa na kubonyeza kwa kidole, jambo ambalo limewafanya wateja kuweka matumaini yao kwa S21, ambayo Taifa Leo imeiorodhesha kama mojawapo ya miundo bora kuwahi kutokea katika historia ya ulimwengu.

 

You can share this post!

Tutakuwa tumedhibiti kero ya nzige kufikia Juni 2021...

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Fasili ya lugha kama nyenzo ya...