Michezo

Hatimaye Timbe aonjeshwa ligi ya Uingereza huku timu yake ya Reading ikishinda

February 15th, 2020 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

AYUB Masika Timbe amepata kionjo cha Ligi ya Daraja la Pili nchini Uingereza baada ya kuchezeshwa kama mchezaji wa akiba timu yake ya Reading ikiwalipua 3-0 wenyeji Sheffield Wednesday uwanjani Hillsborough, Jumamosi.

Timbe, ambaye alijiunga na klabu hiyo ya zamani hapo Januari 31, 2020, alijaza nafasi ya Oviemuno Ejaria dakika ya 86.

Wakenya walikuwa wamelalamika Reading kutomchezesha dhidi ya Cardiff kwenye Kombe la FA (Februari 4) na Hull (Feberuari 8) na West Brom (Februari 12) wakitisha kuacha kushabikia timu hiyo na kudai kuwa haikuwa ikipata ushindi kwa sababu ya kutojumuisha winga huyo Mkenya katika kikosi cha siku ya mechi.

Reading, ambayo haikuwa imeshinda mechi sita zilizopita ligini, ilivuna ushidi dhidi ya Sheffield Wednesday kupitia mabao ya kiungo wa Ivory Coast Yakou Meite, mshambuliaji wa Romania George Puscas na mvamizi Sam Baldock aliyepachika penalti baada ya beki Osaze Urhoghide kuangusha Mzimbabwe Farai Rinomhota ndani ya kisanduku.

Reading inshikilia nafasi ya 15 kwa alama 42 kwenye ligi hiyo ya klabu 24 baada ya ushindi huo muhimu nayo Sheffield Wednesday iko katika nafasi ya 12 alama mbili mbele. Timbe yuko Reading kwa mkopo kutoka Beijing Renhe inyoshiriki Ligi ya Daraja ya Pili nchini Uchina hadi mwisho wa msimu huu.

Naye Clarke Oduor alikuwa kwenye kiti timu yake ya Barnsley ikicharaza wenyeji Fulham 3-0 katika lihgi hii uwanjani Craven Cottage kupitia mabao mawili ya Cauley Woodrow, moja penalti, na Jacob Brown. Barnsley inavuta mkia kwa alama 28, ingawa imejirejesha katika vita vya kukwepa kuangukiwa na shoka baada ya ushindi.

Beki Oduor alijiunga na Barnsley kutoka timu ya Leeds United Under-23 mwezi Agosti 2019.

Baada ya kuibuka Mchezaji Bora wa Barnsley wa mwezi wa Januari, ripoti zinadai kuwa Leeds inaweza kutafuta huduma zake tena kutatua matatizo yake katika idara ya nyuma.