Habari Mseto

Hatimaye ‘Uhuru wa Umoja’ apewa gari aliloahidiwa

September 5th, 2020 2 min read

Na PETER MBURU

MWANAMUME ambaye amepata umaarufu mkubwa kwa wiki kadha sasa, kwa sababu ya kufanana sana na Rais Uhuru Kenyatta, jana alipokea rasmi zawadi ya gari kutoka kwa kampuni moja jijini Nairobi.

Bw Michael Njogo, anayejulikana maarufu kama “Uhunye wa Umoja” alipokea gari hilo katika makao makuu ya kampuni ya Maridady Motors kwenye barabara ya Kiambu, huku akiahidi Wakenya kuwa atalitumia kupanua biashara zake na kujitafutia riziki.

Alipewa gari la thamani ya Sh700,000, akiahidi kufanya nalo kazi za kusafirisha watu (teksi) na biashara nyingine, na kuapa kuwa hatafanya makosa kama ya Bw Martin Kamotho (Githeri Man) ambaye alipata umaarufu wa siku chache kisha akarejelea maisha ya umasikini.

“Hili ndilo gari nilijichagulia mwenyewe. Saa hii nikipewa gari kubwa kisha niende nililalishe hapo kwa ploti halitanisaidia kitu. Hili ambalo nimechukua, hata naweza kubeba wateja nalo kama Uber,” akasema Bw Njogo.

Vilevile, alionyesha kuwa na ari ya kuzidi kukwea kwenda juu zaidi, akisema huu ni mwanzo tu.

“Naanza chini nikienda juu. Mimi si ‘Githeri Man’. Mimi ni mwanabiashara na siwezi kuanzishiwa biashara kwa Sh700,000 halafu nishuke. Naenda juu sasa,” akasema.

Githeriman ni jina alilobatizwa Martin Kamotho Njenga, ambaye wakati wa Uchaguzi Mkuu wa 2017 alipigwa picha akiwa amebeba githeri katika kituo cha kura cha Shule ya Msingi ya Imara, eneo la Kayole, Nairobi.

Hata baada ya kutuzwa na Rais Kenyatta na kupata sifa tele, aliingilia uraibu wa pombe na ulevi mwingine kiasi kwamba mara kwa mara hajitambui.

Ni kutokana na kufeli kwa Githeriman ambapo kampuni ya Maridady Motors ililazimika kumpa ushauri Bw Njogo kuhusu jinsi ya kuendesha biashara.Wakuu wa kampuni hiyo walisema walitaka kuhakikisha kuwa atatumia gari lenyewe ipasavyo.

Walikanusha madai kuwa ni wao walioamua kumpa Bw Njogo gari dogo, badala ya kumwacha achague mwenyewe lile alilotaka.

“Amepokea mafunzo hata kuhusu la kufanya anapofeli katika biashara. Imekuwa safari ya hatua nyingi,” akasema mmoja wa wasimamizi wa Maridady.

Lakini walikiri kuwa sababu ya pekee ya kumzawidi Bw Njogo ni kwa kuwa anafanana sana na Rais Kenyatta na kusema walivutiwa na mapenzi yake kwa biashara ya teksi, ambayo kama kampuni wamekuwa wakiinua.

“Tuliamua kutafuta mtu mmoja mwenye uhitaji na kumsaidia mwaka huu kama jukumu letu la kusaidia jamii kila mwaka,” akasema afisa huyo.

Bw Njogo alianza kupata umaarufu katika mitandao ya kijamii wiki kadhaa zilizopita, baada ya picha zake kusambaa mitandaoni, hali yake ya kufanana sana na Rais Kenyatta ikiwavutia wengi.Baadaye alianza kuhojiwa na kueleza kuhusu maisha yake, nazo baadhi ya kampuni zikaanza kumtafuta ili kujijenga kibiashara, kwa kutumia sura yake.

“Sasa kuna uwezekano kuwa ukiitisha Uber utabebwa na mimi. Utabebwa na Uhunye,” Bw Njogo akasema.

Alikuwa ameandamana na mkewe, Cynthia kupokea gari hilo, ambaye kwa machache tu alisema, “Nimemleta achukue zawadi yake kwa kuwa pale atasaidikia pia mimi nitasaidika.”