Kimataifa

Hatua za Ariel Henry kutaka kuyaponda magenge Haiti zamsukuma kona mbaya

March 12th, 2024 2 min read

WANDERI KAMAU Na MASHIRIKA

HATUA ya Waziri Mkuu wa Haiti Ariel Henry kutangaza kujiuzulu mnamo Jumatatu, imezua maswali kuhusu ikiwa ziara yake kuelekea nchini Kenya mwezi Februari ilikuwa njia ya kutoroka nchini humo.

Henry alitangaza kujiuzulu Jumatatu, baada ya kuelekezewa shinikizo kali na magenge ya uhalifu, yaliyomtaka kujiuzulu, la sivyo asirejee katika taifa hilo.

Tangu alipoondoka Kenya kurejea nchini mwake wiki iliyopita, Bw Henry amekuwa katika nchi ya Puerto Rico, iliyo pia katika ukanda wa Carribean.

Chini ya uongozi wa Jimmy ‘Barbeque’ Cherizier, makundi hayo yalikuwa yameapa kuzidisha uasi dhidi ya serikali, ikiwa kiongozi huyo hangejiuzulu.

Kulingana na makubaliano ambayo yamekuwepo, Henry alifaa kujiuzulu Februari, baada ya kuhudumu kama Waziri Mkuu tangu 2021, kufuatia mauaji ya aliyekuwa rais wa taifa hilo, Jovenel Moise.

Licha ya kutangaza kujiuzulu, uamuzi wa Henry utakuwa rasmi baada ya kubuniwa kwa baraza maalum la mpito na uteuzi wa mtu atakayechukua nafasi yake kwa muda.

Afisa mmoja wa ngazi za juu wa serikali ya Amerika, alisema kuwa Henry alijiuzulu nafasi hiyo mnamo Ijumaa, ijapokuwa hakuwasilisha barua ya kujiuzulu kwa baraza lake la mawaziri hadi Jumatatu jioni.

Henry alikuwa amesafiri Kenya mwishoni mwa Februari, kutafuta usaidizi wa kiusalama kutoka jamii ya kimataifa kuyakabili magenge ya uhalifu, ambayo yamekuwa yakiendeleza vitendo vya ukatili nchini humo.

Alipoondoka, ghasia ziliongezeka katika jiji kuu la taifa hilo, Port-au-Prince, hali iliyomwacha kwenye njiapanda.

Tangu alipochukua uongozi mnamo 2021, kiongozi huyo amekuwa akiahirisha maandalizi ya chaguzi, akilalamikia ukosefu wa usalama.

Alikuwa ameahidi angeng’atuka uongozini kufikia Februari 7.

Je, ni akina nani watakuwa kwenye baraza la mpito?

Baraza hilo  litawajumuisha waangalizi wawili na wanachama saba watakaowakilisha jamii na makundi mbalimbali nchini humo.

Wakati wa kipindi cha mpito, baraza hilo litakuwa likitekeleza majukumu fulani yanayoweza kutekelezwa na rais, japo lazima maamuzi yake yapigiwe kura na kupitishwa na watu wengi.

Baraza hilo pia litamteua waziri mkuu wa mpito, baraza la mawaziri la mpito, kutia saini maagizo muhimu ya serikali na kubuni baraza la mpito la uchaguzi, ambalo litaandaa uchaguzi wa kwanza nchini humo tangu 2016.