Habari

Hatujali sura ya masponsa bora wawe na pesa nyingi – Wanafunzi

January 27th, 2020 2 min read

Na NASIBO KABALE

WANAFUNZI wa kike katika vyuo vikuu nchini wamefichua kwamba huwa hawajali jinsi sura ya mwanamume inavyokaa wanapotafuta ‘masponsa’, mradi tu mwanamume huyo awe na pesa zitakazowapa maisha ya kifahari.

Kulingana na utafifiti, wasichana hao hutarajia kupokea takriban Sh50,000 kila mwezi kutoka kwa ‘masponsa’.

Utafiti huo uliofanywa na shirika la Busara Center for Behavioural Economics, umeonyesha kwamba kati ya wanafunzi watano wa kike vyuoni, mmoja ana uhusiano wa kimapenzi na mwanamume wa umri wa juu ambaye jukumu lake kuu ni kufadhili mahitaji ya kifedha.

Shirika hilo liligundua kuwa wakati wanafunzi wanapopekua mitandao ya kijamii kutafuta wanaume, wao hutazama zaidi uwezo wake wa kifedha kuliko sura.

“Mapato yalitiliwa uzito kwa alama ambazo mwanamume alipewa ili awe ‘sponsa’. Aliye na mapato ya juu alipata alama zaidi. Walio na magari waliongezwa alama pia,” ikasema ripoti hiyo.

Kando na hayo, wasichana waliohojiwa walisema huwa hawajali kama mwanamume sponsa ana mke na familia. Hata hivyo, wangetilia maanani suala hilo kama mwanamume ni mpenzi wao wa kawaida.

Lakini wengi walifichua huwa wanaona aibu kufichulia watu kuhusu uhusiano wao wa kimapenzi na masponsa ambao kwa kawaida huwa ni wazee sana kuwaliko.

Utafiti huo ulisema uhusiano huo umebainika kuwapa wasichana nafasi ya kupata pesa, burudani na kufadhili maisha yao wanapokuwa chuoni ili waishi kwa starehe.

Yale wanayopata kutoka kwa wanaume hao ni usafiri katika maeneo ambayo kwa kawaida hawangefika wakiwa wanafunzi, burudani na nafasi ya kununua chochote watakacho ikiwemo kukodisha vyumba katika mitaa ya kifahari wakiwa wangali wanafunzi.

Utafiti huo ulishirikisha wanafunzi wa kike walio na umri kati ya miaka 18 na 24 kutoka vyuo vikuu mbalimbali jijini Nairobi.

Hata hivyo, kwa jumla ilibainika wanawake hutarajia kupewa pesa wanaposhiriki ngono na mwanamume, iwe ni mpenzi wao au sponsa.

Tofauti ya matarajio kutoka kwa wapenzi na masponsa ni kwamba masponsa hutarajiwa kutoa pesa nyingi zaidi na zawadi nono kuliko inavyotarajiwa kutoka kwa wapenzi wa kawaida.