Habari za Kitaifa

Hatujalipwa! Kilio cha familia za polisi waliotumwa Haiti


FAMILIA za maafisa wa polisi wa Kenya waliotumwa Haiti zimelalamika kwamba bado hazijalipwa tangu walipoanza oparesheni ya kudumisha amani nchini humo.

Haya yamejiri miezi miwili baada ya Balozi wa Amerika Antony Blinken kuagiza kutolewa kwa Sh14.1 bilioni kufadhili oparesheni hiyo iliyoidhinishwa na Umoja wa Mataifa (UN).

Fedha hizo vilevile zinadhamiriwa kununua vifaa vya kijeshi kwenye handaki zilizopo katika jiji kuu la Port-au-Prince, ambapo polisi wa Kenya wanafanyia shughuli zao.

Katika mahojiano na jamaa wa familia kadhaa za polisi wa Kenya waliochelea kutajwa wakihofia unyanyapaa, walisimulia masaibu ya kifedha kutokana na kucheleweshewa malipo.

Wengine walilalamika kuwa, huku shule zikifunguliwa Jumatatu, Agosti 26, 2024 hawana uwezo wa kulipa karo na kuwanunulia watoto wao vifaa vinavyohitajika kwa muhula wa tatu wakati mitihani ya kitaifa inatarajiwa kuanza.

“Shule zinafunguliwa na kila mara ninapowasiliana naye, ninachopata tu ni, bado hatujalipwa,” alisema jamaa mmoja wa familia.

Alishangaa ni nini mume wake anafanya Haiti ilhali hawezi kugharamia mahitaji licha ya kuhakikishiwa wangepata malipo ya ziada.

Jamaa wa afisa mwingine wa polisi alisema watoto wake huenda wakakosa kurejea shule ikiwa hawatalipwa fedha hizo.

“Kusema kweli tuna tatizo hapa kwa sababu hata kugharamikia chakula na mahitaji mengineyo kumeanza kuwa changamoto,” zilisema duru.

Taifa Dijitali imethibitisha tatizo hilo na baadhi ya maafisa wa polisi walio Haiti ambao, hata hivyo, hawakutaka kulijadili kwa kina na badala yake kutuelekeza kwa familia zao Kenya.

Kikosi cha kwanza cha polisi wa Kenya kiliwasili Haiti Juni 25, 2024 baada ya kupokezwa bendera ya Kenya siku iliyotangulia na Rais William Ruto.

Kikosi cha pili kilitumwa Julai 16, 2024 na kuongeza idadi hiyo kuwa 394 lakini bado hawajatimia maafisa 1,000 waliopangiwa kutumwa.

Maafisa hao wanajumuisha kikosi cha kukabiliana na ghasia (GSU), Kikosi Maalum na Kikosi cha Kupiga Doria Mpakani (BPU).

Tulipowasiliana naye kuhusu malalamishi hayo, Kaimu Inspekta Jenerali Mkuu wa Polisi, Gilbert Masengeli alisema “maafisa watapata malipo yao kwa wakati.”

Katibu katika Wizara ya Masuala ya Kigeni, Korir Sing’oei na Mshauri wa rais kuhusu Usalama wa Kitaifa, Monicah Juma, hawakujibu maswali yetu.

Wiki iliyopita, kundi linalofahamika kama Caribbean Community (CARICOM) lilitoa taarifa likisema oparesheni hiyo inagubikwa na changamoto tele ikiwemo upungufu wa vifaa, uhaba wa fedha na kuchelewesha kubuni taasisi za serikali.

Timu hiyo ilialikwa na Mkuu wa Baraza la Rais kuhusu Mageuzi Haiti, Leslie Voltaire.

Katika mikutano hiyo iliyofanyika kati ya Agosti 11 na 16 na Waziri Mkuu wa Haiti, Garry Conille, timu hiyo iliorodhesha changamoto zinazokabili Polisi wa Haiti (HNP) na vikosi vya polisi wa Kenya.