Habari Mseto

Hatujamtimua Chiloba, tunamtia adabu tu – IEBC

September 25th, 2018 1 min read

Na PETER MBURU

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) Jumanne imepinga kauli kuwa afisa wake mkuu mtendaji (CEO) Ezra Chiloba ambaye yuko kwenye likizo ya lazima amefutwa kazi, ikisisitiza kuwa bado mchakato wa kumuadhibu Bw Chiloba unaendelea.

Hii ilikuwa baada ya gazeti la The Star kuchapisha kuwa tume hiyo ilimfuta kazi afisa huyo, ndipo Jumanne asubuhi ikaja kuweka mambo wazi, ikipinga kamwe kufanya hivyo.

“Si kweli kuwa CEO Ezra Chiloba, ambaye yuko katika likizo ya lazima, amefutwa zkazi. Ukweli ni kuwa mchakato wa adhabu unaendelea na tume itatoa uamuzi wa kina kuhusiana na suala hilo,” IEBC @IEBCKenya ikasema Jumanne.

Ripoti hizi sasa zinakuja wakati Bw Chiloba amekuwa akikumbana na matatizo tele ya kikazi, yakiwemo kufungiwa nje licha ya korti wiki chache zilizopita kuamuru arejee kazini.

Baada ya uamuzi huo wa korti, mwenyekiti wa tume hiyo alitangaza kuwa Bw Chiloba alikuwa ametimuliwa tena na hata vifuli vya milango ya afisa yake vikabadilishwa.

Majuzi afisa huyo alikuwa ameenda katika afisa za tume lakini akarudi baada ya kupata afisa yake ikiwa imefungwa na kukosa kupatana na mwenyekiti wa tume hiyo Wafula Chebukati.

Haifahamiki kama maneno ya tume hiyo kuwa “tume itatoa uamuzi wa kina kuhusiana na suala hilo” unaweza kuwa kidokezo kuwa mwishowe hatima ya Bw Chiloba itaishia kufutwa kwake kazi.