Hatukutengewa fedha za referenda, IEBC yafafanua

Hatukutengewa fedha za referenda, IEBC yafafanua

Na CHARLES WASONGA

TUME Huru ya Uchaguzi na Mipaka (IEBC) imefafanua kuwa Sh14.5 bilioni ilizotengewa katika bajeti iliyosomwa na Waziri wa Fedha Ukur Yatani sio za kufadhili kura ya maamuzi.

Kaimu Afisa Mkuu Mtendaji wa tume hiyo Hussein Marjan Ijumaa alinukuliwa akisema kuwa fedha hizo ni za kufadhili maandalizi ya uchaguzi mkuu ujao na kuendeleza shughuli za kawaida za IEBC.“Fedha za kura ya maamuzi sio sehemu ya Sh14.5 bilioni ambazo IEBC imetangewa katika bajeti ya mwaka wa kifedha wa 2021/2022.

Fedha hizo ni za kufadhili shughuli zetu ya kiusimamizi na matayarisho ya uchaguzi mkuu ujao,” akaeleza.Kauli yake inashahibiana na yake kiongozi wa wachache katika bunge la kitaifa John Mbadi ambaye alisema IEBC haingetengewa fedha za kura ya maamuzi “kwa sababu ya suala kuhusu uhalali wa Mswada wa BBI ungali mahakamani”.

“Kamati ya Bajeti haingetenga fedha za kufadhili kura ya maamuz kwa sababu hatima ya shughuli hiyo bado haijaamuliwa na mahakama. Hatuwez kutenga fedha kwa shughuli ambayo hatujui kama itaendelea ua la.

Sehemu kubwa ya fedha zilizotengewa IEBC zitatumiwa katika shughuli za usajili wa wapiga kura wapya, ununuzi wa vifaa vya uchaguzi na shughuli nyinginezo,” Bw Mbadi akaambia Taifa Leo baada ya usomaji wa bajeti katika majengo ya bunge, Alhamisi.

Kesi ya kupinga kuharamishwa kwa Mswada wa marekebisho ya Katiba kupitia mpango wa maridhiano (BBI) inatarajiwa kuanza kusikizwa wiki ijato katika Mahakama ya Rufaa.Rais wa Mahakama hiyo Daniel Musinga ambaye aliapishwa Ijumaa anatarajiwa kuteua jopo la majaji saba watakaosikiza kuamua kesi hiyo.

Kesi hiyo imewasilishwa na Rais Uhuru Kenyatta, Kiongozi wa ODM Raila Odinga na IEBCWanapinga uamuzi wa majaji matano wa Mahakama Kuu ambao mwezi jana walitaja mchakato huo kama ulikiuka Katiba na hivyo haramu.Uamuzi huo ulitolewa na majaji Joel Ngugi, George Odunga, Chache Mwita na Bi Teresia Matheka.

Mwaka jana Mwenyekiti wa IEBC Wafula Chebukati aliwaambia wabunge wanachama wa Kamati ya Bunge Kuhusu Haki na Masuala ya Kikatiba (JLAC) kwamba tume hiyo inahitaji Sh14 bilioni kuendesha kura ya maamuzi.Ijumaa, Bw Marjan alithibitisha kuwa kiasi hicho cha fedha ndicho kinahitajika kufadhili maandalizi na uendeshaji wa kura ya maamuzi.

“Tulikuwa tumewasilisha bajeti na mipango yetu ya maandalizi ya kura ya maamuzi kwa Hazina ya Kitaifa kabla ya mahakama kuu kutoa uamuzi wa kusitisha shughuli ya marekebisho ya Katiba.” akaeleza.

Bw Marjan alitoa hakikisho kwamba endapo Mahakama ya Rufaa itabatilisha uamuzi wa Mahakama Kuu, IEBC itakuwa tayari kuendesha kura ya maamuzi “mradi hazina ya kitaifa itupe fedha.”

  • Tags

You can share this post!

Miradi ya Uhuru Nyanza inavyotishia kuchimbia Raila kaburi...

Uchaguzi wafanyika kundi maarufu likisusia