Michezo

HATUMTAKI: Chelsea wachoka kocha wao, wataka abanduke

May 23rd, 2019 2 min read

Na MASHIRIKA

LONDON, Uingereza

BAADHI ya wachezaji wa Chelsea wametishia kuagana na klabu hiyo iwapo kocha Maurizio Sarri atasalia kwenye usukani msimu ujao.

Ripoti jijini hapa zimesema kwamba mastaa kadhaa wa kikosi cha kwanza hawafurahii mbinu za kocha huyo, hata baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL), mbali na kutinga fainali ya Europa League.

Kadhalika, mashabiki wameeleza kutoridhishwa kwao na ukufunzi wa kocha huyo ambaye alipewa mamlaka baada ya Antonio Conte kutimuliwa kufuatia vuta nikuvute baina yake na wachezaji.

Sarri alishambuliwa vikali kufuatia kichapo kikubwa dhidi ya Manchester City na pia Watford katika msimu huu uliomalizika, ingawa alianza kuandikisha matokeo mazuri katika mechi zilizofuatia.

Kuna uvumi kwamba wakuu wa klabu hiyo tayari wamepanga kumuondoa kocha huyo wa zamani wa Napoli licha bila kuzingatia matokeo ya fainali ya Europa League, kwa lengo la kuzuia wachezaji kuondoka.

Kiungo mahiri mstaafu Franck Lampard aliyechezea klabu hiyo kwa miaka 13 pamoja na aliyekuwa kocha wa Juventus, Massimiliano Allegri ni miongoni mwa wakufunzi wanaowekewa nafasi kubwa kwenye vita vya kuchukua nafasi hiyo hasa baada ya habari kuibuka kwamba tayari Allegri ameanza kujifunza Kiingereza.

Kishindo

Chelsea watamaliza msimu kwa kishindo iwapo wataibuka na ushindi dhidi ya Arsenal mjini Baku kwenye fainali ya Europa League hapo Mei 29.

Klabu hiyo ya Stamford Bridge imepata afueni baada ya kiungo matata N’golo Kante kupata nafuu na kurejea mazoezini.

Ni habari njema kwa kocha Sarri ambaye alikuwa amebakia na viungo watatu pekee; Jorginho, Mateo Kovacic na Ross Barkley baada ya Ruben Loftus-Cheek kuumia juma lililopita kwenye mechi ya kirafiki dhidi ya New England Revolution ya Amerika ambapo Chelsea ilishinda kwa 3-0.

Kwingineko, staa Christian Pulisic ambaye ataanza kuchezea Chelsea baada ya msimu huu kumalizika amesema angefurahia zaidi kucheza pamoja na Eden Hazard ambaye anatarajiwa kujiunga na Real Madrid.

Raia huyo wa Croatia anayechezea Borussia Dortmund ya Ujerumani amekuwa mali ya Chelsea tangu mapema mwaka huu, lakini ataanza kuwahudumia baada ya msimu huu kumalizika.

Akizungumza kwenye mahojiano kupitia kituo kimoja cha vipindi vya michezo, Pulisic alisema, “Ninaamini kila mtu anatamani kucheza naye (Hazard), ni mchezaji wa kiwango cha juu. Itakuwa fursa nzuri kucheza naye pamoja. Nitaingia kikosini na kucheza kwa bidii hasa iwapo nitashirikishwa naye kikkosini.

“Nimemshuhudia kupitia kwa televisheni na kwa kweli ni mchezaji wa kutamaniwa kutokana na umahiri wake awapo uwanjani.”
Pulisic alisajiliwa na Chelsea mnamo Junuari kwa kiasi cha Sh8.9 bilioni, lakini aliendelea kuchezea Dortmund kwa mkopo.