Michezo

Hatumuuzi Coutihno licha ya kumlisha benchi, Barca yasema

January 8th, 2019 1 min read

NA CECIL ODONGO

NYOTA wa Barcelona Philipe Coutinho amehakikishiwa kwamba yupo kwenye mpango wa baadaye wa timu hiyo  japo amekuwa akilishwa benchi baada ya miguu yake kuingia kutu, mwaka moja tangu atue uwanja wa Camp Nou.

Coutinho, 26 ameshindwa kabisa kudhihirisha makali yake langoni mwa wapinzani na kuthibitisha kwamba hela nyingi zilizofanikisha usajili wake kutoka Liverpool Januari 2018 hazikupotea bure.

Mwanasoka huyo hajaanza mechi yoyote tangu Disemba2 na alijukumiwa uwanjani na kocha Ernesto Valvade kwa muda wa dakika saba tu wakati wa ushindi wa 2-1 dhidi ya Getafe siku ya Jumapili.

Hata hivyo, Mkurugenzi Mkuu wa Barcelona Guillermo Amor amesema kwamba mchezaji huyo ana kandarasi ya muda mrefu na Barca itakayomwezesha kung’aa sana siku zijazo wala timu hiyo haina mpango wa kumuuza.

“Coutinho ni mchezaji mwenye tajriba pana na kati ya wachezaji bora barani Uropa. Yeye kila mara yupo tayari kutandaza soka uwanjani kwa dakika tano au tisini,”

“Yeye ni mchezaji anayefikiria sana kuhusu timu asiyejawa na ubinafsi au kulalamikia muda mchache uwanjani. Barca walimsaini kwasababu ya ubora wake duniani na tunatarajia mengi kutoka kwake,” akasema Amor.

Kati ya mara 22 alizowajibika msimu huu, ameanza mechi 15. Vile vile amechangia  mabao matano na  akasaidia kuyafunga manne katika ligi ya Uhispania La Liga na mchuano wa kuwania Klabu Bingwa Barani Uropa.