Habari Mseto

Hatuna budi kujituma zaidi – maoni

December 31st, 2019 2 min read

Na LAWRENCE ONGARO

WAFANYABIASHARA kadha wameendelea na biashara zao kama kawaida licha ya watu kuendelea na pilikapilika za sherehe za sikukuu.

Hata ingawa watu wamekuwa wachache mjini Thika, baadhi ya maduka yameonekana yamefunguliwa biashara ikiendelea huku wauzaji nguo na bidhaa nyingine wakiendelea na biashara zao kama kawaida.

Bw John Maina ambaye huuza nguo za mitumba kando ya barabara na maduka, anasema yeye alisherehekea sikukuu Desemba 25, 2019, lakini kesho yake alikuwa anaendelea na biashara yake kama kawaida.

“Ama kwa hakika mambo ni magumu wakati huu, tukikosa kujikakamua wakati huu, bila shaka Januari 2020, itatupiga chenga kiasi. Kwa hivyo ni vyema kujua ya kwamba majukumu ni mengi katika mwezi huo,” alisema Bw Maina.

Nauli

Katika kituo cha magari cha Thika leo Jumanne matatu za kwenda sehemu mbalimbali zimetoza nauli ya kawaida kwa sababu sio wasafiri wengi walionekana kituoni hapo.

“Sisi tumeamua kutoza nauli ya kawaida kwa sababu tunajua vyema wasafiri wengi walikosa kwenda kusherehekea sikukuu mwaka huu wa 2019,” amesema Bw James Mwangi ambaye ndiye kondakta wa kutoza wasafiri katika ruti ya Meru na Nyahururu. Nauli ya kwenda Meru ni Sh450 lakini mara nyingi msimu wa sherehe za Krismasi na Mwaka Mpya huwa Sh700. Halafu Nyahururu abiria hutozwa kawaida Sh650 lakini wakati wa sikukuu ni hadi Sh800,” amesema Bw Mwangi.

Wasafiri waliokuwa wakirejea nyumbani kutoka sikukuu mjini Thika walikuwa ni wachache Desemba 31, 2019. Hata nauli ilikuwa in kawaida. Picha/ Lawrence Ongaro

Watu wengi waliohojiwa wamesema ya kwamba lengo lao kuu lilikuwa kujipanga kwa Januari 2020 kwa sababu ndipo kuna mahitaji mengi ya kutatua na kugharimia.

Peter Mwangi ambaye huuza simu za rununu anasema hata maana ya sikukuu imekosa ladha tena kwa sababu kwa mtazamo wake, “hakuna pesa kabisa na kwa hivyo kila mmoja sharti ajikakamue ili angalau kupata kitu kidogo.”

“Tunaelewa mwezi wa Januari huwa ni mwezi wa mawazo chungu nzima. Kila mmoja atakuwa mbioni kutafuta karo ya shule hasa wale wanaojiandaa kuwapeleka watoto wao kujiunga na kidato cha kwanza,” amesema Bw Mwangi.

Bi Mary Wangari ambaye huuza nyanya, vitunguu na ndizi, katika soko kuu la Jamhuri mjini Thika, anasema alilazimika kuuza bidhaa zake hasa wakati huu wa sikukuu ili kupata karo za mtoto wake anayejiunga na kidato cha kwanza.

“Sisi kama wazazi tuko na majukumu mengi sana hasa mwezi wa Januari ambapo kila mmoja yumo mbioni kuona ya kwamba mtoto wake anarejea shuleni na pia kulipia madeni mengi ya mikopo,” amesema Bi Wangari.

Magari ya usafiri hasa ya kwenda Embu hadi Meru yamelipisha kama kawaida kutoka Thika baada ya sikukuu.

Bi Margaret Muthoni aliyesafiri Embu Desemba 29, 2019 alilipishwa nauli ya Sh250 kwa sababu sio watu wengi walisafiri kwenda kutangamana na wenzao mashinani kwa sikukuu.