Habari MsetoSiasa

Hatuna nia ya kumtimua Uhuru Ikulu – Seneta Cherargei

January 8th, 2019 2 min read

ONYANGO K’ONYANGO na WYCLIFF KIPSANG

VIONGOZI wa Jubilee wanaoegemea upande Naibu Rais William Ruto wamekanusha madai kwamba wanapanga njama za kumwondoa Rais Uhuru Kenyatta mamlakani kupitia kura bungeni, ikiwa Dkt Ruto atazuiwa kuwania urais mnamo 2022.

“Tunaamini katika uongozi wa Rais Kenyatta na hakuna hata mmoja wetu aliye na mipango kama hiyo. Watu wanapaswa kujitenga na madai kama hayo yasiyo na msingi wowote,” akasema Seneta wa Nandi Samson Cherargei.

Viongozi mbalimbali wa ukanda wa Kaskazini mwa Bonde la Ufa jana waliunga mkono kujiuzulu kwa aliyekuwa Naibu Mwenyekiti wa Jubilee (JP) David Murathe, ila wakashinikiza kuandaliwa kwa uchaguzi mpya wa maafisa wakuu katika chama hicho.

“Lazima tufanye uchaguzi wa chama kulingana na Sheria ya Vyama vya Kisiasa. Hili litatusaidia katika kuimarisha mipango inayohusu mustakabali wake,” akasema Bw Cherargei.

Wabunge Daniel Rono (Keiyo Kusini) na Caleb Kositany (Soy) walisema kwamba wanataka uongozi mpya katika chama hicho ili kukiimarisha ielekeapo mwaka 2022.

“Chama hiki kitaandaa kikao cha wajumbe wote ili kupanga wakati ambao tutafanya uchaguzi kuwachagua viongozi wapya. Hili litawafanya wafuasi wetu kujihisi kuwa wamiliki wa chama,” akasema Bw Kositany, aliye pia Naibu Katibu Mkuu wa chama hicho.

Mbunge wa Kapseret Oscar Sudi pia alimwomba Rais Kenyatta kuitisha uchaguzi wa chama ili kuwaondoa maafisa ambao wanazua migawanyiko na uhasama miongoni mwa viongozi.

Bw Sudi aliunga mkono kujizulu kwa Bw Murathe, huku akimtaka Katibu Mkuu wa Jubilee Raphael Tuju kujiuzulu pia.

Mbunge huyo alidai kwamba mabw Tuju na Murathe wanatumiwa na watu wenye ushawishi kuzua mgawanyiko chamani, ili kumzuia Dkt Ruto kumrithi Rais Kenyatta mnamo 2022.

Wabunge hao walisema kwamba Bw Ruto atakabiliana na kiongozi yeyote ambaye atajitokeza kupigania tikiti ya Jubilee kuwania urais. Walisema kwamba wanaamini katika demokrasia, kama ilivyo katika katiba ya JP.

“Tuju anapaswa kumleta mwaniaji wake bila kuogopa chochote. Hii ni kwa kuwa Dkt Ruto hahitaji uteuzi wowote wa moja kwa moja, ila tunaamini kwamba atashinda katika chaguzi zote,” akasema Bw Rono.

Wiki iliyopita, Bw Ruto alisema kuwa hatapewa tiketi ya moja kwa moja na chama kuwania urais.